NA ZAINAB IDDY
KIUNGO mpya wa Yanga, Kabamba Tshishimbi, ametua nchini tayari kuungana na wenzake kisiwani Pemba, baada ya Wanajangwani hao kumalizana na klabu yake ya Mbabane ya Swaziland.
Tshishimbi, ambaye alishasaini mkataba wa miaka miwili na Yanga, alishindwa kutangazwa na klabu hiyo kama ilivyokuwa kwa wengine, kutokana na kuwa na mkataba na Mbabane, lakini kwa sasa pande hizo mbili zimemalizana.
Ili kumtumia kiungo huyo, Yanga walitakiwa kutoa Dola 20,000 za Marekani (sawa na Sh milioni 43.7) ili kuvunja mkataba wake.
Taarifa ambazo BINGWA imezipata jana kutoka ndani ya Yanga, zinasema klabu hiyo imemalizana na Mbabane.
“Kikwazo kilikuwa ni fedha za kuvunja mkataba wake, lakini tayari tumekamilisha hilo,” alisema mtoa habari wetu huyo.
Lakini, BINGWA ilipomtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, Hussen Nyika, alidai kuwa kilichokuwa kikikwamisha ujio wa kiungo huyo ni suala la hati yake ya kusafiria (passport) kubakiza muda mfupi kabla ya kumalizika na kwamba suala la fedha walishalimaliza.
“Jana (juzi) alikabidhiwa (hati ya kusafiria) mpya ya muda mrefu, lakini pia amekabidhiwa tiketi, hivyo atawasili leo (jana), ingawa siwezi kusema ni muda gani.
“Mara baada ya kuwasili Tanzania, haraka atakwenda kuungana na wenzake Pemba kwaajili ya kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, akianza na ile ya ufunguzi baina yetu na Simba, Agosti 23, mwaka huu,” alisema.