NA HUSSEIN OMAR
KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, ameonekana kumpa kazi maalumu beki wake, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, baada ya jana kuonekana kucheza kwa utulivu wa hali ya juu kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Pemba.
Katika mchezo huo ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0, Ninja alicheza dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuonyesha kiwango cha hali ya juu kwa kukaba, kunyang’anya mipira na kuweza kuwazuia vyema washambuliaji wa Jamhuri.
Awali, Ninja jina lake lilikuwa kama kituko kwa mashabiki wa soka hasa wale wa Simba, baada ya kujifunga kwenye moja ya mchezo wa kirafiki ambao Yanga walilala bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, lakini pia akisababisha penalti walipocheza na Singida United.
Lakini kiwango alichokionyesha kwenye mchezo wa juzi Pemba, kimefuta kabisa matukio yote mabaya ya beki huyo na sasa Lwandamina ameoneka kumwamini baada ya kuonyesha kiwango kizuri na kufuata maelekezo yote aliyokuwa akipewa na bosi wake huyo.
Ninja ambaye juzi alicheza na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alicheza kwa uelewano mkubwa na beki huyo wa kati na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kuanza kumkubali.
Lakini pamoja na yote hayo, wapo mashabiki wa Yanga wanaotamani beki huyo apangwe kesho dhidi ya Simba ili kuwadhibiti wachezaji wasumbufu wa Wekundu wa Msimbazi hao, ikiwamo kutibua mipango yao ya kusaka mabao.
Akizungumza kuhusu kiwango cha beki huyo, Lwandamina alisema ni beki mzuri ambaye anaendelea kuimarika siku hadi siku hivyo ana matumaini makubwa naye.
“Tulikuwa kwenye kozi na sasa tumemaliza, nimeridhishwa na viwango vya wachezaji wangu, sina mengi zaidi ya kusema tukutane kesho Uwanja wa Taifa,” alisema Lwandamina.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanatarajia kurejea leo jijini Dar es Salam baada ya kumaliza kambi ya wiki moja Pemba kujiandaa na mchezo wa kesho wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.