LONDON, England
STRAIKA Diego Costa juzi alisisitiza kuwa hataweza kurejea tena kwenye klabu yake Chelsea na huku akisema kuwa anasaka kupata kibarua mahali pengine.
Straika huyo mtata alienguliwa kwenye kikosi cha kwanza cha Antonio Conte tangu mwanzoni mwa majira haya ya joto na kipindi hicho chote amekuwa akikitumia akiwa katika mapumziko nchini kwao Brazil.
Wakati dalili za kurejea katika timu yake ya zamani ya Atletico Madrid zikionekana kuwa wazi, lakini kuna mchakato finyu unaoendelea na sasa zimebaki takribani wiki mbili kabla ya dirisha la usajili halijafungwa.
Hali hiyo ndiyo inamfanya Costa aanze kuhangaika kutafuta mahali pa kwenda na tayari ameshatangaza kuwa atajitafutia mwenyewe klabu atakayoichezea kuanzia msimu ujao.
“Wakala wangu ameshasema kwamba, Chelsea wanataka kitu ambacho Atletico hawawezi kuwa nacho,” staa huyo aliuambia mtandao wa ESPN Brasil.
Kutokana na hali hiyo, BINGWA limeangalia ni klabu ipi ambayo inaweza kuwa mbadala wa Costa.
- Everton
Kocha wa Everton, Ronald Koeman, alisema katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa kuzungumzia mechi za mwishoni mwa wiki kwamba wataomba kumchukua kwa mkopo Costa.
Kauli hiyo inaonekana inaweza kuwa kweli kutokana na kwamba kwa sasa Everton inahitaji straika mwenye nguvu baada ya kumpoteza nyota wake, Romelu Lukaku ambaye amejiunga na Manchester United.
Hata hivyo, licha ya Costa kuonekana bado anahitaji kubaki kwenye michuano ya Ligi Kuu England, lakini tatizo ni kwamba Everton hawataki kulipia gharama zote za mshahara wa Costa katika kipindi chote ambacho atakuwa akiwachezea kwa muda.
Katika maelezo yao Toffes, wanadai kuwa wanataka kumchukua Costa kwa mkopo hadi Januari mwakani ambapo watamwachia ili akakamilishe usajili wake Atletico Madrid baada ya timu hiyo kumaliza kifungo chake cha kuzuiwa kutosajili.
- AC Milan
Iliripotiwa mwanzoni mwa majira haya ya joto kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya AC Milan wapo kwenye mazungumzo na uongozi wa Chelsea ili iwauzie Costa.
Milan, ambao wameshampoteza straika wao, Carlos Bacca, aliyekwenda kujiunga na Villarreal hadi sasa wameshatumikia kitita cha pauni milioni 170 kwa ajili ya kununua wachezaji wapya.
Vinara hao kwa sasa wana kiu ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Serie A msimu huu ili kumaliza ufalme wa Juventus, lakini wanachokikosa ni straika mwenye makali ya kuwawezesha kufanya hivyo, jambo ambalo pia Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo, Marco Fassone, alilikiri mwezi uliopita.
Mbali na timu hiyo pia mahasimu wao, Inter Milan, vile vile nao walikuwa wakiripotiwa kummezea mate straika huyo na hivyo panaweza kuwa mahali pake.
- Ligi ya China (Chinese Super League)
Kutimkia katika michuano ya Ligi Kuu ya China, Chinese Super League, mara zote kumekuwa kukitajwa kuwa ndiko atakapokimbilia Costa na huku mwishoni mwa Januari mwaka huu timu ya Tianjin Quanjian, ikiripotiwa kuwa mbioni kumnasa staa huyo.
Hata hivyo, mchakato huo ulikwama kabla ya dirisha hilo dogo la usajili halijafungwa na hivyo kumfanya Costa ashindwe kuondoka.
Hata hivyo, endapo Costa atashindwa kupata timu katika kipindi cha wiki mbili zijazo milango itakuwa wazi kwake kwenda China kabla ya msimu ujao haujaanza.
- Atletico Madrid
Licha ya ndoto za Costa za kutaka kurejea tena Atletico kutokamilika hadi sasa, lakini pengine kuna siku hali hiyo inaweza ikatokea.
Kwa sasa vinara hao wa soka Hispania wamezuiwa kusajili hadi Januari mwakani, jambo ambalo linawafanya washindwe kufanya kitu chochote kuhusu Costa.
Lakini jambo hilo linaweza kukamilika endapo straika huyo atapata pa kujishikiza kwa muda hadi ifikapo Januari.
- Sport Recife
Hii ni klabu nyingine ambayo Costa anaweza kwenda na kisha akapumzisha akili yake akiwa nchini kwao Brazil.
Kwa sasa Sport Recife inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Brazilian Serie A hivyo haitakuwa vibaya kwa staa huyo kujiunga nayo.