ZAINAB IDDY NA EZEKIEL TENDWA
LICHA ya Simba kuibuka na ushindi dhidi ya mahasimu wao Yanga na kutwaa Ngao ya Jamii, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja, amesema hawakuridhishwa na kiwango cha wachezaji wao.
Pambano hilo la kukata na shoka lilipigwa jana katika Dimba la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Simba waliibuka kidedea kwa kushinda mikwaju ya penalti 5-4.
Katika mechi hiyo, Simba waliwaonyesha jeuri watani wao wa jadi Yanga na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya pili wakikutana wenyewe kwa wenyewe, ambapo Wanajangwani hao pia wana rekodi ya kulibeba kombe hilo mara mbili mbele ya Wekundu wa Msimbazi hao.
Akizungumza baada ya mechi hiyo jana, kocha huyo raia wa Uganda alisema mipango yao ilikuwa ni kumaliza mpira ndani ya dakika 90 na si zaidi.
“Kitendo cha kumaliza dakikia 90 bila kupata bao inaonyesha wazi kwamba eneo la umaliziaji bado lina tatizo, hivyo tunakwenda kufanya kazi kuhakikisha tatizo hilo halijirudii tena,” alisema.
Mayanja aliongeza kuwa benchi la ufundi litajipanga upya kuhakikisha tatizo la kukosa mabao ndani ya dakika 90 halijitokezi katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.