MANCHESTER, England
STRAIKA mkongwe kwenye soka, Zlatan Ibrahimovic, ameibuka na video ikimwonesha jinsi gani alivyo fiti kwa sasa baada ya kupona jeraha lake la goti.
Video hiyo iliyokuwepo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, ilimwonesha Ibrahimovic akilipiga fuko kubwa la kupigia ngumi kwa kutumia mguu wa kulia na wa kushoto.
Mbwembwe hizo zinakuja baada ya kuuguza goti lake la kulia aliloumia dhidi ya Anderlecht katika mchezo wa Ligi ya Europa msimu uliopita, maumivu yaliyomkosesha mechi zote zilizosalia.
Video hiyo ilidhihirisha kweli ‘mnyama’ amerejea kwa kasi kwani nguvu alizokuwa akitumia kulitandika teke fuko hilo ni nyingi sana ukilinganisha na jinsi alivyoumia.
Ilitajwa kwamba, madaktari walimshauri Ibrahimovic apumzike vya kutosha ili kulifanya goti lake hilo lipone vizuri, lakini ameonesha ukaidi. Hata hivyo, ndiyo kawaida yake.
Straika huyo wa zamani wa klabu ya PSG anahusishwa kurudi dimbani na kuichezea tena Man United iliyomtema.
Iliripotiwa kuwa kocha wa United, Jose Mourinho, anajiandaa kumchukua tena na moja ya kazi atakayompa ni ukocha.
Mourinho alithibitisha kuwa klabu ipo kwenye mazungumzo na Ibrahimovic ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa kama mfungaji bora wa United katika Ligi Kuu England na mabao yake 17.