MICHAEL MAURUS NA MARIAM SHABANI (TUDARCO)
KABLA na baada ya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya timu yake na Yanga, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alikuwa kikaangoni kutokana na kiwango cha safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi hao kiasi cha kufikiria kufungashiwa virago.
Watu wa Simba walikuwa hawana imani naye katika suala zima la kuinoa safu ya ushambuliaji, ambayo ilishindwa kufunga mabao mengi katika michezo yao ya kirafiki takribani minne, ikiambulia mabao matatu tu.
Na katika mchezo wa Ngao ya Jamii, pamoja na kikosi chake kuaminika kusheheni wachezaji wa kiwango cha juu, bado Simba ilishindwa kufunga hata ‘bao la kuotea’ ndani ya dakika 90 za kawaida.
Mbaya zaidi, watu wa Simba waliamini Yanga haikuwa na beki imara ya kuweza kuwazuia washambuliaji wao wanaoongozwa na Mganda Emmanuel Okwi, lakini pia ikiwa na winga hatari, Shiza Kichuya.
Ndio maana pamoja na timu yao kubeba Ngao ya Jamii kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4, watu wa Simba hawakuonekana kuwa na furaha wakiamini hawakustahili kufika hatua ya mikwaju ya penalti.
Hapo ndipo presha ya kutimuliwa kwa Omog ilipozidi hali iliyolifanya BINGWA kumtafuta Mcameroon huyo kufahamu mtazamo wake juu ya kinachoendelea Simba dhidi yake, hasa baada ya habari kuwa viongozi wake walikuwa wamempa mechi nne.
Omog alisema kuwa anafahamu jinsi ‘anavyowindwa’ na kwamba yupo tayari kwa lolote, ikiwamo kutimuliwa akidai kuwa akiwa kama kocha, amekuwa akijiandaa kwa lolote dhidi yake.
Lakini juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Omog alifanikiwa kuruka kihunzi cha kwanza dhidi ya lawama ya ukame wa mabao kwa washambuliaji wake, baada ya Simba kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting.
Ushindi huo ni wazi utakuwa umetoa ahueni kwa kocha huyo na iwapo kikosi chake kitaendelea kupata matokeo mazuri kwenye mechi zijazo za ligi, wazo la kutimuliwa halitakuwapo tena.
Presha ya watu wa Simba inatokana na ukweli kuwa klabu hiyo imesota kwa takribani miaka mitano bila taji la Ligi Kuu Bara, huku wakiwakodolea macho watani wao wa jadi, Yanga wakijinafasi japo wamekuwa wakikabiliwa na upinzani kutoka kwa Azam.
Ndani ya muda huo wa miaka mitano, Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne, wa msimu uliopita ukiwa ni wa tatu mfululizo.