ZAITUNI KIBWANA NA ZAINAB IDDY
WASHAMBULIAJI wa Yanga, Donald Ngoma na Ibrahim Ajib, wameongezewa nguvu ili waweze kuifungia timu hiyo mabao, hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msimu mpya wa ligi hiyo wa 2017/18, ulianza mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Yanga walipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli ya Iringa, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilionekana kukosa makali na kushindwa kufunga bao lolote lile pamoja na kupata nafasi kadhaa za kufanya hivyo.
Kwa kutambua hilo, benchi la ufundi la Yanga limeamua kuongeza mshambuliaji mmoja wa kati kusaidiana na Ajib na Ngoma kuzichachafya safu za ulinzi za timu pinzani na hivyo kufunga mabao kadiri watakavyopata nafasi.
Mchezaji aliyeongezwa ni Antony Matheo hivyo kuunda umoja utakaofahamika kama NAM, yaani Ngoma, Ajib na Mathew.
Kabla ya umoja huo, tayari Yanga ina CTN, yaani Chinrwa (Obrey), Tambwe (Amissi) na Ngoma, huku pia wakiwa na ACN (Ajib, Chirwa, Ngoma) na ATN (Ajib, Tambwe na Ngoma).
Ukiachana na utambulisho wa Mathew katika mazoezi ya jana, pia benchi la ufundi lilimwongeza Abadallah Shaibu ‘Ninja’ katika safu ya ulinzi wa kati ambapo alicheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, huku pembeni kushoto kukiwa na Haji Mwinyi na kulia Juma Abdul.
Kwa upande wa viungo, benchi la ufundi la Yanga chini ya kamanda wao, George Lwandamina, lilikuwa likiunda safu hatari ya kiungo iliyowahusisha Thaban Kamusoko, Pappy Kabamba Tshishimbi, Said Juma Makapu, Marka Edward, huku mawinga wakiwa ni Yusuph Mhilu, Emmanuel Martin na Juma Mahadhi.
Wengine waliohusika katika programu ya mazoezi ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ni Andrew Vincent ‘Dante’, Hasssan Ramadhani ‘Kessy’, Pato Ngonyani na wengineo.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema kwa sasa wanayafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo yao ya nyuma.
“Nafahamu tunakabiliwa na michezo ya ugenini, ukizingatia awali tulicheza na timu ambayo imepanda daraja na mechi inayofuata na wao vilevile ni wageni na wameweza kuonyesha uwezo mzuri, hivyo lazima tujihami ili tukapambane na kupata pointi tatu muhimu,” alisema.