NA ZAINAB IDDY
WAKATI Simba wakitarajia kucheza na Azam Septemba 6, mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja, amesema wataibuka na ushindi bila mshambuliaji wao tegemeo, Emmanuel Okwi.
Akizungumza na BINGWA jana, Mayanja alisema wana uwezo wa kuifunga Azam si chini ya mabao matatu bila nyota huyo aliyekwenda kuitumia timu yake ya Taifa ya Uganda, inayokabiliwa na michuano ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazopigwa Urusi mwakani.
Mayanja alisema katika mchezo wao na Azam watamkosa beki wao, Jjuuko Murshid aliyeungana na Okwi kwenye kikosi cha Taifa cha nchi yao kitakachocheza na Misri.
Alisema kukosekana kwa wachezaji hao hakutaathiri uwezo wa timu hiyo, kwani wana kikosi kipana.
“Ingawa wachezaji hao wawili ni muhimu katika mechi yetu dhidi ya Azam kutokana na ushindani wa ligi, lakini tayari tunaziandaa silaha nyingine,” alisema Mayanja.
Hata hivyo, wataingia uwanjani kuvaana na Azam wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa msimu uliopita, lakini walifungwa bao 1-0 waliporudia.
Simba walianza msimu mpya kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-4, baada ya kutofungana ndani ya dakika 90 katika mchezo uliochezwa Agosti 23, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hiyo ilianza Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, katika mechi iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.