NA WINFRIDA MTOI
KIPA wa Simba, Aishi Manula, amemvutia Kocha wa timu ya Taifa ya Botswana, David Bright, baada ya kuonyesha kiwango cha juu alipoidakia Taifa Stars katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Taifa Stars ilishinda mabao 2-0 dhidi ya wageni wao kwenye mchezo huo uliopo katika kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la mpira wa miguu Duniani (Fifa).
Bright aliridhishwa na uwezo wa Manula na kuahidi atamtafutia timu ya kudakia inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Bright alisema kiwango cha Manula ni kikubwa, anastahili kucheza soka nchi yoyote na kiwango hicho ndicho kimemfanya atamani kumtafutia timu inayocheza Ligi Kuu Afrika Kusini.
“Kwa kweli nimevutiwa na kazi aliyoifanya kipa ni nzuri, kiwango chake ni cha juu hadi amenivutia kumtafutia timu ya kucheza Afrika Kusini,” alisema.
Akizungumzia mchezo huo, alikiri kikosi chake kuzidiwa licha ya kucheza vizuri na alisema sababu walikutana kwa muda mchache kujiandaa na aliwakosa baadhi ya nyota wake.