Monday, October 26, 2020

SAFI SANA AMUNIKE KUWATOA USHAMBA BOCCO, KICHUYA, NYONI, *DOMAYO, KIDUKU, NGALEMA, KIHIMBWA MSIMWANGUSHE MNIGERIA*

Must Read

Fati aweka rekodi Barcelona

CATALUNYA, Hispania ANSU Fati ameweka rekodi ya mchezaji kinda wa kwanza kufunga mabao...

Lampard amshika mkono Silva

MANCHESTER, England KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard, amesema atamtumia, Thiago Silva, katika mechi nyingi msimu huu licha ya...

Tuchel awatolea uvivu Mbappe, Neymar

PARIS, Ufaransa KOCHA wa PSG, Thomas Tuchel, amechukizwa na kiwango kibovu walichoonyesha mastaa wa timu hiyo, Kylian...

NA MICHAEL MAURUS


PAMOJA na Tanzania kutajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye vipaji lukuki vya soka, ikiwamo mashabiki ‘waliochizika’ vilivyo na mchezo huo, bado Taifa hilo limeshindwa kutamba katika anga ya kimataifa.
Ukiachana na soka la kimataifa, hata kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja, nchi yetu imeshindwa kujitambulisha ‘ughaibuni’ tofauti na ilivyo kwa nchi kama Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon, Togo, Misri, Morocco, Tunisia na nyinginezo zenye nyota wanaotamba Ulaya na kwingineko.
Kuna wachezaji ambao wamezitambulisha vilivyo nchi zao kila kona ya dunia kutokana na cheche zao walizozionyesha au wanazoendelea kuzionyesha wakiwa wanazitumikia timu mbalimbali nje ya mipaka ya mataifa yao.
Leo hii majina la wachezaji kama Roger Milla, Samuel Eto’o, Rigobert Song (Cameroon), Didier Drogba, Yaya Toure (Ivory Coast), Abeid Pele (Ghana), Nwankwo Kanu, Jay Jay Okocha, Benni McCarthy (A. Kusini), Mohammed Salah (Misri), Victor Wanyama (Kenya) na wengineo, wamefanikiwa vilivyo kuzitangaza nchi zao kutokana na jinsi walivyovitendea haki vipaji vyao ‘Majuu’.
Japo Tanzania ilianza mapema kutamba katika soka kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, mwishoni mwa miaka ya 1970 hadi mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1980, lakini imejikuta ikipitwa na nchi zilizokuwa nyuma yake.
Baada ya Tanzania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1980, ilikuwa ikiogopwa mno na kila timu iliyopangwa kucheza nayo, tofauti na ilivyo sasa ambayo imekuwa kimbilio ikiaminika kama ‘kichwa cha mwendawazimu’.
Enzi hizo, timu za Taifa za Uganda, Zambia, Malawi, Ethiopia, Sudan na Kenya zilikuwa zikiihofia mno Taifa Stars tofauti na ilivyo kwa sasa.
Angalau Tanzania ilianza kurejea kwenye ramani ya soka baada ya kuwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
Enzi zake, Maximo aliunda timu imara iliyotoa upinzani wa hali ya juu hata ilipokutana na timu za mataifa yaliyopiga hatua katika soka Afrika, zikiwamo Cameroon, Ivory Coast, Senegal, Sudan, Uganda na nyinginezo.
Mathalani, katika michuano ya kufuzu fainali za Chan mwaka 2009, Stars chini ya Maximo, ilifanikiwa kuzifunga timu za Kenya (2-1) katika mchezo wa kwanza na timu hizo ziliporudiana, kikosi cha Mbrazil huyo kikashinda bao 1-0.
Baada ya hapo, Maximo aliwaongoza vijana wake kuichapa Uganda mabao 2-0 kabla ya kuipata sare ya bao 1-1 waliporudiana.
Hatimaye, Stars ilijikuta ikivaana na Sudan na kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza na ziliporudiana, ilishinda bao 1-0 na hivyo kufuzu fainali hizo za Chan zinazowahusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani.
Katika fainali hizo zilizofanyika nchini Ivory Coast kuanzia Februari 22, hadi Machi 8, 2009, Stars ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Senegal, kabla ya kuichapa Ivory Coast bao 1-0 na mwishowe kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia na hivyo kuaga michuano hiyo.
Tangu enzi hizo za Stars ya Maximo, soka la Tanzania limekuwa likidorora kiasi cha kujikuta ikiwa vibonde mbele ya mataifa kama Kenya, Uganda, Sudan, Zambia, Msumbiji na nyinginezo za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, lakini pia Kusini, Kaskazini na Magharibi.
Swali kubwa ambalo limekuwa likitawala miongoni mwa wadau wa soka nchini ni juu ya wapi tunapokosea. Leo hii tuna mchezaji mmoja tu anayetamba Ulaya katika ligi inayotambulika, Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, huku pia tukiringia Simon Msuva anayefanya mambo Difaa El Jadida ya Morocco.
Japo wachambuzi wa mambo ya soka wamekuwa wakiwatupia lawama viongozi wa soka nchini kwa kutokuwa na mikakati thabiti ya kulifikisha mbali soka letu, lakini pia wachezaji wenyewe wamekuwa ni chanzo kikubwa cha hilo.
Pamoja na kufahamu kuwa soka ndio maisha yao tofauti na ilivyokuwa zamani wakati wachezaji walipokuwa wakicheza soka kama burudani na sehemu ya kuiweka miili yao fiti, lakini walifanya mambo makubwa mno.
Hilo ni tofauti kabisa na sasa wakati ambao soka umekuwa ni mchezo unaolipa mno duniani kiasi cha kuwafanya wachezaji wanaotamba Ulaya kulipwa mabilioni ya fedha kwa huduma ya muda mfupi mno.
Japo wanalifahamu hilo, leo hii unaweza kumwona mchezaji wa soka akivimba kichwa kutokana na mafanikio kiduchu mno, huku akisahau jinsi akina Drogba walivyovuna mabilioni ya fedha kupitia miguu yao kiasi cha kuitangaza nchi yake, lakini pia akiwekeza katika miradi mbalimbali Ivory Coast na kwingineko.
Leo hii tunasubiri kumwona Samatta akitamba katika ligi kubwa Ulaya kama za England, Hispania, Italia, Ufaransa au hata Ujerumani kutokana na jinsi anavyokitendea haki kipaji chake.
Hakika mafanikio ya Samatta hayajaja hivi hivi, bali yametokana na kujituma kwake uwanjani, lakini kubwa zaidi akizingatia nidhamu ya soka kuanzia ndani hadi nje ya uwanja kama ilivyo kwa wachezaji wengi waliofanikiwa duniani kote, wakiwamo akina Ronaldo de Lima (Brazil), aliyetoka katika familia duni mno, David Beckham (England), Thiery Henry (Ufaransa) na wengineo.
Katika kudhihirisha jinsi wachezaji wetu wasivyojielewa, ni jana tu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amewatoa kikosini mwake nyota kadhaa ambao Watanzania walikuwa wakiwategemea kuipeperusha vema Bendera ya Taifa katika michuano ya kuwania kufuzu fainali za Afcon 2019.
Wachezaji hao ni John Bocco, Shomari Kapombe, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga, Jonas Mkude na Erasto Nyoni wote wakiwa ni wa Simba.
Nyota hao wanaounda kikosi cha kwanza cha Simba, wameenguliwa Stars kutokana na kushindwa kuripoti kambini kwa wakati na badala yao, Amunike amewaita kikosini Paul Ngalema (Lipuli), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), David Mwantika (Azam FC), Frank Domayo (Azam FC), Kelvin Sabato ‘Kiduku’ (Mtibwa Sugar) na Ali Abdulkadir (Lipuli) kuziba nafasi za wenzao hao.
Ikumbukwe kuwa kikosi cha Taifa Stars kimeweka kambi tangu juzi katika Hoteli ya Seascap, jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019) dhidi ya Uganda itakayopigwa Septemba 8, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau, alisema waliahirisha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ili programu ya Amunike iweze kutekelezwa kama alivyohitaji.
Alisema kocha alitoa utaratibu wake wa wachezaji kuripoti kambini kwa wale wa Simba na Azam, siku ya mwisho kuwa jana, huku wa Yanga wakitakiwa kufanya hivyo mara watakapowasili nchini wakitokea Rwanda walikokwenda kuvaana na Rayon Sports ya huko jana jioni.
Kidau alisema wachezaji wanaocheza nje ya nchi, wataanza kuripoti kambini Septemba 4, mwaka huu kutokana na majukumu ya timu zao.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba, alisema Amunike aliyewahi kutamba na kikosi cha Nigeria ‘Super Eagle’ katika fainali za Kombe la Dunia 1994 zilizofanyika nchini Marekani, aliwasiliana na viongozi wa Simba kuwataka wawapigie simu wachezaji wao kuwasisitiza kuripoti kambini kwa wakati aliopanga, lakini hadi jana saa 12:30 asubuhi ambao ni muda wa mwisho waliopewa, walikuwa hawajafika.
Mbali ya wachezaji hao, Kidau alisema Meneja wa Simba, Robert Richard na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Hamis Kisiwa, watafikishwa katika Kamati ya Maadili ya TFF Jumamosi kujieleza kwa sababu walipelekewa taarifa mapema za kuwaruhusu wachezaji wao.
Ama kwa hakika, Amunike anastahili pongezi kwa msimamo wake huo kwani kwa kocha wa ‘kuungaunga’, asingethubutu kuwaacha wachezaji kama hao, tena kutokana na timu inayoshikilia ubingwa ambayo nyuma yake, kuna mfanyabiashara mkubwa na maarufu mno Afrika, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Labda kupitia msimamo huu wa Amunike aliyeichezea Nigeria mechi 27, akifunga mabao tisa, unaweza kuwazindua wachezaji wa Tanzania na kuanza kujitambua hali inayoweza kuishuhudia nchi yetu ikiwa na akina Samatta kibao Ulaya, tena kwenye timu kubwa kama Manchester United, Chelsea, Arsenal, Barcelona, Real Madrid, AC Milan, Juventus na nyinginezo.
Kwa muda mrefu, suala la utovu wa nidhamu na kutofuata miiko ya soka, vimekuwa vikiwatesa mno wachezaji wetu na mwisho wa siku kushindwa kufikia malengo yao na matumaini ya Watanzania juu yao na soka la Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, bila shaka wachezaji waliochukua nafasi za wakali hao wa Simba, yaani Ngalema na wenzake, hawatamwangusha Amunike aliyezikosa fainali za Kombe la Dunia 1998 kutokana na matatizo ya goti yaliyokuwa yakimkabili.
Wachezaji hao walioitwa kuchukua nafasi za wenzao, wafahamu kuwa wana deni kubwa mno kwa Amunike aliyeiongoza Super Eagles kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Tunisia mwaka 1994 na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka huo, lakini pia akifunga bao la ushindi katika mchezo wa fainali ya michuano ya Olimpiki mwaka 1996.
Hongera sana Amunike kwa msimamo wake, wengine tuanzie alipoishia ili kulifikisha soka letu pale linapostahili

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Fati aweka rekodi Barcelona

CATALUNYA, Hispania ANSU Fati ameweka rekodi ya mchezaji kinda wa kwanza kufunga mabao...

Lampard amshika mkono Silva

MANCHESTER, England KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard, amesema atamtumia, Thiago Silva, katika mechi nyingi msimu huu licha ya kuwa na umri wa miaka...

Tuchel awatolea uvivu Mbappe, Neymar

PARIS, Ufaransa KOCHA wa PSG, Thomas Tuchel, amechukizwa na kiwango kibovu walichoonyesha mastaa wa timu hiyo, Kylian Mbappe na Neymar, kwenye mechi...

IBRA:Kifaa kipya Konde Gang aliyetembea kwa mguu kumwinda Harmonize

NA BRIGHITER MASAKI UKITAJA vijana wanaofanya vizuri katika mziki wa bongo fleva, huwezi kukosa kumtaja msanii chipukizi anayefahamika zaidi...

Jay-Z: Mama aliingilia bifu langu na Nas

-Z: Mama aliingilia bifu langu na Nas New York, Marekani HAKUNA shabiki wa Hip hop asiyelifahamu...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -