Thursday, October 22, 2020

EVER BANEGA, INUA MIKONO JUU, MUNGU NI WAKO NA NI WETU SOTE

Must Read

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu...

NA HALID MTUMBUKA

NDANI ya kikosi cha Inter Milan anaishi binadamu mmoja anayefanya kazi yake ipasavyo. Anaibeba ipasavyo Inter Milan kwenye mabega yake, licha ya kuelemewa na mzigo mzito wa kukimbiwa na mafanikio waliyokuwa nayo miaka ya nyuma.

Binadamu huyu inawezekana akawa amekosa bahati kabisa hapa duniani, jicho la bahati mbele ya dunia halijaiona miguu yake na shughuli yake nzito anayoifanya ndani ya Inter Milan. Kama angekuwa na bahati asingebahatika tena lakini huyu binadamu hatambui uwepo wa bahati chini ya jua.

Binadamu huyu alizaliwa nchini Argentina miaka 28 iliyopita, anaitwa Ever Banega.

Akilini kwa mwanadamu yeyote yule hutawaliwa na kumbukumbu nzuri kadhaa, kumbukumbu ambazo ni ngumu sana kupotea.

Unakumbuka mchezo wa fainali ya Ligi ya Europa msimu uliopita kati ya Inter Milan dhidi ya Liverpool? Huyu ndiye aliyeinyanyasa ipasavyo safu ya kiungo ya Liverpool.

Alikuwa akipiga pasi zilizofika kwa usahihi, aliijua ipasavyo kazi yake, alikuwa tofauti maradufu, miguu tu ndiyo iliyokuwa ikiongea kwenye fainali hiyo.

Banega ni hatari mno anapolifikia lango la timu pinzani, anajieleza hasa kwa kupiga pasi zenye uhakika wa kufika kwa aliyemlenga, ana macho zaidi ya macho ya kawaida, anaona zaidi ya anavyoona akiwa nje ya mchezo.

Kuna wakati bahati duniani nayo ipo, ukiyaruhusu macho yako kutengeneza taswira za kumtafuta kiungo mshambuliaji aliyekamilika barani Ulaya, hutaweza kumpata popote pale isipokuwa Inter Milan.

Kiungo mwenyewe hatakuwa mwingine zaidi ya Ever Banega. Macho yangu hayadanganyi, hakuna kiungo mshambuliaji aliyekamilika barani Ulaya zaidi ya Ever Banega.

Sijui kwanini wale Tottenham Hotspur hawamuoni! Nawaza tu Christian Eriksen na Delle Alli wanapolimiliki eneo la ushambuliaji, Eric Dier na Victor Wanyama wanaposimama kwenye majukumu ya ulinzi, Ever Banega kwa kazi yake nzuri angeweza kuweka uwiano katikati yao.

Nimewaza tu kwa maandishi. Jicho la Inter halikukosea kufanya maamuzi ya uhamisho wake wa bure kutoka Sevilla. Banega amekosa bahati tu, kipaji amezaliwa nacho kwenye damu yake.

Amekosa bahati kwa sababu Inter anayoishi ndani yake si Inter inayostahili kumiliki kipaji cha Banega. Inter si klabu yenye mafanikio tena siku hizi, imekimbiwa na mafanikio wakati huu.

Anguko la kiuchumi limeanguka na mafanikio yao, Inter ya leo haivutii tena wachezaji wenye vipaji kwenda kusakata gozi la ng’ombe kwenye viunga vyake.

Inter ya leo kuishi katika nafasi ya 11 juu ya Cagliari, Genoa na Sassuolo si jambo la kuishangaza dunia. Dunia haiwashangai hivi sasa, ni kawaida tu.

Inter ya leo kutokuwa na uwiano mzuri kati ya safu ya ulinzi na safu ya ushambuliaji si jambo la kushangaza, haina fedha kama zamani, ndiyo maana inaruhusu kufungwa mengi kuliko hata Fiorentina.

Inawezekana vipi kiungo mwenye uzuri wa kushughulika na mipira ya adhabu na mashuti ya mbali kama Banega akastahili kucheza kwenye aina hii ya timu?

Banega inua mikono juu uombe kwa muumba wako, usiwaamini wale wanasayansi wasioamini uwepo wa Mungu licha ya magumu mengi wanayopitia kwenye majaribio yao, Mungu ni wako na ni wetu sote. Banega inua mikono juu, Mungu anasubiri maombi yako.

Ameshaona uwezo wako, ameshazishuhudia juhudi zako za kupenda sana soka la kusaka mpira katika kila kona ya uwanja, anasubiri maombi yako tu, ayajibu.

Naiheshimu sana Inter Milan, kuna nyota wa dunia waliowahi kuufanya uwanja mzima kusimama, mmoja wapo ni Luis Figo pale alipocheza mchezo wake wa mwisho mwaka 2009.

Mwaka huohuo, Atalanta waliadhibiwa mabao 4-3 na kuifanya Inter kutwaa taji la 17 la Scudetto. Hii ilikuwa Inter iliyotengeneza penzi lililochanua kwenye kila moyo wa shabiki wake.

Inter hii iliishi vyema kwenye vifua vya wanaume, ilimfanya kila aliyeitwa shabiki wake kuchanua tabasamu pana usoni mwake.

Nakumbuka masimu wa 2004/05 Juventus walivyobariki Inter watwae Italian Super Cup, nakumbuka pia, tabasamu la Sinisa Mihajlovic na Dejan Stankovic wakati wakitwaa Coppa Italia.

Naikumbuka Inter ya Roberto Mancini, nikiilinganisha na hii ya Frank De Boer, moyo wangu hauna sababu ya kumtaka Banega amuombe Mungu wake aidha Inter irudi kwenye zama zake au yeye akaishi mahala anapostahili.

Kazi yake ni kubwa mno, kiwango chake kinamruhusu kucheza kwenye timu ya inayomstahili. Kwanini asiende kuishi huko? Kwanini asiiache Inter?

Kipaji chake kina hadhi ya kuonekana kwenye timu yenye hadhi.

Unaweza kujiuliza ni yeye tu ambaye anacheza kwenye timu inayomfunika kipaji chake? Ngoja nikwambie, kuna baadhi ya wachezaji wana viwango vinavyostahili kuonekana kwenye timu yenye hadhi zao.

Jiulize kuhusu uwezo alionao winga wa Kijerumani, Julian Draxler anastahili kucheza kwenye kikosi cha Wolfsburg?

Jibu lako likiwa ndiyo mwenyewe ameshasema anahitaji kutimka kwenye timu hiyo.

Ni binadamu gani anayeweza kuruhusu nguvu zake zitumike kwenye sehemu isiyostahili?

Nyakati zimebadilika sana siku hizi, thamani ya utu ilishanunuliwa na pesa, hakuna thamani ya utu tena.

Hata mpira ulishahama siku nyingi kutoka kwenye burudani hadi kuwa biashara kubwa, ni pesa iliyofanya yote hayo. Tuamini tu nyakati zimebadilika!

Banega kwanini asibadilike na yeye? Kwanini asifuate upepo utakapoelekea? Ninachokiamini ndicho kilichopo hapa, miaka 28 ndiyo wakati sahihi wa kucheza soka mahali penye hadhi ya sawa na thamani ya kipaji kilichobebwa na miguu ya mtu husika.

Maisha mema Banega, kumbuka usitarajie kuiona Inter ikinyakua mataji makubwa msimu huu, ikitokea nafasi nikukute umeichangamkia. Alamsiki.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya wanamuziki wa Tanzania ambao miongoni...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara  (VPL), utakaochezwa leo...

Mugalu atema cheche Simba

NA ASHA KIGUNDULA MSHAMBULIAJI wa Simba, Chris Mugalu, amesema wanakwenda mkoani Rukwa kupambana na kupata ushindi katika mchezo wao...

Malale aitisha Yanga

NA ZAINAB IDDY KOCHA Mkuu wa timu ya Polisi Tanzania, Malale Hamsini, amezisikia sifa za kocha mpya wa Yanga,...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -