LONDON, England
KLABU ya Arsenal imedhamiria kuwapa adhabu mashabiki wao walionunua tiketi za msimu kama watashindwa kuwa na mahudhurio mazuri uwanjani baada ya kuumizwa na suala la siti za uwanja wa Emirates kuwa tupu, huku tiketi nyingi zikiwa hazijatumika na mashabiki wao au hata kuziachia kupitia mfumo maalum wa mabadiliko wa klabu hiyo.
Na leo Jumatatu, bodi ya Arsenal itakaa mezani kuangalia uwezekano wa kuwaadhibu mashabiki walionunua tiketi za msimu na kushindwa kuhudhuria mechi mbalimbali.
Msemaji wa mashabiki wa Arsenal, Tim Payton, aliliambia gazeti la Telegraph: “Kama mtu atatumia tiketi yake mara chache kwa mwaka sasa itabidi apewe onyo na baada ya hapo hatakuwa na uwezo wa kununua tiketi hiyo msimu ujao.
“Jambo hili litatatulika tu. Watu watakapokuwa wengi kwenye mechi moja hiyo ina maana kwamba ni wapya na viti vitaongezwa uwanjani, lakini pia itazidisha uhamasishaji kwa wachezaji pindi watakapokuwa wanapambana.
“Kama Arsenal itakuwa inawaza tu kuhusu pesa, basi bodi isingejisumbua kufuatilia ni mashabiki wangapi walionunua tiketi za msimu wamehudhuria uwanjani. Kama wanapendezwa na hali iliyopo uwanjani na kuwa mfano kwa mashabiki wachanga kupenda kuhudhuria mechi basi wanatakiwa kutopuuzia suala hili,” alisema Payton.