NA CLARA ALPHONCE
SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Simba, Hamis Kilomoni, kudai hawautambui Mkutano Mkuu wa klabu hiyo ulioitishwa na viongozi, Rais Evans Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’, wamemuunga mkono kuukataa mkutano huo.
Mkutano Mkuu wa Simba umepangwa kufanyika Agosti 12, wakati ule wa mabadiliko ya katiba ni Agosti 20, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Kilomoni alisema baada ya kupata malalamiko ya wanachama waliomuita makao makuu ya klabu, aliamua kwenda kuwaona viongozi hao waliopo mahabusu Keko na kuwaeleza mambo yanayoendelea, ambapo walikubaliana mkutano usifanyike.
“Kwa sasa Simba imegawanyika katika makundi mawili ya Simba Asili na Wahindi, jambo ambalo ni hatari kwa klabu, kwani litaleta mpasuko mkubwa,” alisema Kilomoni.
Alisema Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo imekiuka katiba kwa kuwateua wajumbe ambao hawakustahili kuongoza na pia hawana uwezo wa kuitisha mkutano mkuu.
“Katiba ya Simba inasema mkutano mkuu wa klabu utaitishwa na rais na kama hayupo ni makamu wake, lakini wasipokuwepo wote basi ni mjumbe aliyekaa kwa muda mrefu ndani ya klabu.
“Ukiangalia waliopewa madaraka ya kukaimu hawastahili, bali waliostahili ni Kassim Dewji na Zacharia Hanspoppe,” alisema Kilomoni.
Alisema kama viongozi wataendelea kukaidi agizo la Bodi ya Wadhamini ambao pia ni wamiliki wa mali zote za Simba zinazohamishika na zisizohamishika, watakwenda mahakamani kuwashtaki, kwani wasipofanya hivyo nao watashtakiwa na wanachama wa Simba.