NA SAADA SALIM
NAHODHA wa Azam FC, Himid Mao, amewatahadharisha wapinzani wao kwamba, yeyote atakayepambana nao usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, hatatoka salama.
Akizungumza na BINGWA jijini jana, Mao alisema kuwa, wamekuwa na rekodi nzuri wanapotumia uwanja wao huo kucheza mechi usiku, kwa kupata matokeo mazuri tofauti na inavyokuwa mchana.
Mao alitoa kauli hiyo baada ya mechi yao dhidi ya Kagera Sugar, waliyoshinda bao 1-0, shujaa wao akiwa ni Mbaraka Yussuph, aliyecheka na nyavu dakika ya 43, akiunganisha pasi ya Yahya Zayd.
“Usiku ni vizuri, ukizingatia mazingira yapo vizuri, hakuna jua, mchezaji anafanya chochote uwanjani kuhakikisha anaipatia ushindi timu yake,” alisema.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Azam huwa inapata matokeo mazuri inapocheza usiku katika uwanja wao huo wa nyumbani kuliko wanapocheza mchana.
Katika mechi tano za mwisho wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara walizocheza katika uwanja huo usiku, zote waliibuka na ushindi.
Baadhi ya mechi hizo ni dhidi ya Mbao FC waliyoibuka na ushindi wa mabao 3-1, Stand United (2-0), Toto African (2-0), Kagera Sugar (1-0).