NA MWANDISHI WETU
UONGOZI wa klabu ya Azam umechukua uamuzi mgumu baada ya kusitisha mkataba wa benchi lake la ufundi lililokuwa chini ya Kocha Mkuu Mhispania, Zeben Hernandez, kutokana na matokeo mabaya ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Kali Ongala akitajwa kurithi mikoba yake.
Hernandez amekatishiwa mkataba pamoja na wasaidizi wake, Jonas Garcia ambaye alikuwa kocha wa viungo, msaidizi wa kocha huyo, Pablo Borges, kocha wa makipa, Jose Garcia na daktari wa timu hiyo, Sergio Perez.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na viongozi wa Azam kupitia Azam TV, zilieleza makocha hao wametimuliwa baada ya timu hiyo kutoka sare katika mechi mbili mfululizo za mzunguko wa pili wa ligi hiyo dhidi ya African Lyon na Majimaji ya Songea.
Katika mechi ya kwanza ya mzunguko huo, Azam walipata sare kwa African Lyon katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, kabla ya kufungana bao 1-1 na Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Matokeo hayo yalikuwa ni mwendelezo wa Azam kufanya vibaya msimu huu, ambao hadi sasa wameshinda mechi saba, sare sita na kufungwa minne, wakishika nafasi ya nne kutokana na pointi 27.
Pamoja na kufanikiwa kuipa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 katika mechi iliyochezwa Agosti 17 mwaka huu, lakini Hernandez ameonekana kushindwa kuipa mafanikio zaidi timu hiyo ya Chamazi.
Makocha hao wametimuliwa huku wakikabiliwa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Azam wanaonekana kupoteza ushindani wao tangu Hernandez alipoanza kuifundisha timu hiyo, akichukua mikoba ya Stewart Hall, aliyeomba kuachia ngazi.
Hall aliifikisha timu hiyo nafasi ya pili msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara na kuipa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame mwaka jana.
Kocha Mkuu wa Majimaji, Kali Ongala ambaye pia aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo chini ya Hall, anatajwa kushika nafasi ya Wahispania hao kwa muda kabla ya kuchukuliwa kwa kocha wa kudumu hapo baadaye.
Azam pamoja na kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini wanajiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayoanza Februari mwakani.