NA SAADA SALIM,
AZAM imezikejeli Yanga na Simba kuwa zimewasaidia mno katika maandalizi yao ya mechi za kimataifa, baada ya kuwachapa watani hao wa jadi katika mechi tatu zilizopigwa ndani ya mwezi huu.
Timu hiyo ilifanikiwa kuichapa Yanga mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar mapema mwezi huu, kabla ya kuishushia Simba bao 1-0 katika fainali ya michuano hiyo.
Baada ya hapo, Jumamosi ya wiki iliyopita, Azam iliendeleza ubabe wake kwa wakongwe hao wa soka nchini kwa kuichapa Simba bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Na sasa Azam imetamba kuwa baada ya kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Bara, kwa sasa akili zao zote wamezielekeza katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiamini wana uwezo wa kufanya vema.
Azam itacheza hatua ya makundi moja kwa moja dhidi ya mshindi kati ya Mbabane Swallon ya Swaziland na Opara United ya Botswana kati ya Februari 11, 12 na 13, mwaka huu.
Akizungumza na BINGWA jijini jana, kocha wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’, alisema walikuwa na dawa ya kuzimaliza timu hizo na kwamba wamepania vilivyo kuirejesha timu yao katika ubora wake.
Cheche alisema haikuwa kazi rahisi kupata ushindi katika timu hizo kongwe, akiamini mafanikio yao hayo yametokana na jinsi anavyozifahamu timu hizo kongwe tangu alipokuwa mchezaji.
“Simba tayari tulicheza nayo mwanzo haijabadilika sana, mfumo wao waliocheza Unguja ndio ule ule,” alisema.