NA ZAINAB IDDY
AZAM wametenga bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 5.7 kwa ajili ya uendeshaji wa timu yao kwa msimu mmoja wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Bajeti hiyo inaonekana ni kubwa kuliko ya klabu kongwe za Simba na Yanga, ambazo zinatumia chini ya kiasi hicho katika msimu mmoja wa ligi hiyo.
Simba inatumia Sh bilioni 1.2 wakati Yanga wanatumia bilioni 2.5 katika uendeshaji wa timu hizo.
Akizungumza na BINGWA, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, alisema bajeti hiyo inajumuisha masuala yote ya mishahara ya viongozi na wachezaji, lakini kambi na maandalizi kwa ajili ya ligi hiyo.
Kawemba alisema bajeti hiyo itaongezeka wanaposhiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kwa Kagame, Kombe la Shirikisho FA na Kombe la Mapinduzi Zanzibar.
“Bajeti yetu ya mwaka huu ni ya kawaida kwani imegusa maandalizi ya ligi kuu pekee.
Muda mwingine inavuka kiwango hicho kutokana na kuongezeka kwa mahitaji mengine yakiwemo mashindano ya kimataifa,” alisema Kawemba.