BARCELONA, Hispania
SAKATA kuhusu suala la kuondoka nyota wa Barcelona, Neymar, kwenda kujiunga na timu ya Paris Saint-Germains, sasa limechukua sura mpya baada ya mashabiki wa klabu hiyo kuja juu wakimtaka afungashe virago mapema kwa kile wanachodai ni msaliti.
Kwa mujibu wa gazeti la Marca, mashabiki hao walianzisha kasheshe hilo juzi baada ya kutinga nje ya uwanja wao wa Camp Nou, wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ukimtaka nyota huyo aachane na klabu yao na huku mengine yakimuita msaliti.
“Msaliti anatafutwa,” lilieleza moja ya bango lililokuwa limetundikwa nje ya uwanja huo wa Camp: “Wasaliti ni lazima waondoke, Barcelona ni kwa ajili ya wachezaji pekee wanaoipenda jezi yetu,” liliongeza bango jingine.
Hasira hizo za mashabiki zinaripotiwa kupanda zaidi baada ya Neymar kurejea Catalonia bila kueleza juu ya hatima yake ndani ya klabu hiyo.
Juzi pia waandishi wa habari walijitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa ndege wa El Prat wakimsubiri nyota huyo wakati akitokea nchini Dubai, lakini kwa haraka staa huyo mwenye umri wa miaka 25, akaondoka kwa kupitia mlango wa uwani.
Huku msimu mpya ukikaribia kuanza mashabiki wa klabu hiyo ya Catalan walikuwa na kiu ya kutaka kufahamu hatima ya nyota huyo, huku wengine wakiwa na matumaini ataendelea kubaki Camp Nou.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza hatima ya utata wa sakata hilo unatarajiwa kumalizika Jumatatu wiki ijayo baada ya uhamisho wake wa kutoka Barcelona kwenda Paris Saint-Germain, utakapokamilika na pia jana aliruhusiwa kuondoka kwenye kambi ya timu hiyo.