Tuesday, October 27, 2020

BUSUNGU, HATA JIWE LIKIACHA MAPEPE LINAWEZA KUWA DHAHABU

Must Read

Katwila: Sitaidharau Mbeya City

NA VICTORIA GODFREY KOCHA wa timu ya Ihefu, Zuberi Katwila, amesema hawaraidharau  Mbeya City...

Kocha apokea kipigo kwa shingo upande

 NA  VICTORIA GODFREY KOCHA wa timu ya Mwadui, Khalid Adam, amesema amesikitishwa na kipigo...

KMC kumaliza hasira kwa Gwambina

NA WINFRIDA MTOI BAADA ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga, kocha...

NA HALID MTUMBUKA

DON Harvey ni mwanafalsafa aliyewahi kuiambia dunia kwamba chochote ambacho ubongo wa mwanadamu utakipokea na kukiamini, ubongo huo utajilazimisha kukipata. Maneno yanaumba.

Mwanafalsafa huyu alidhamiria kuuonesha ulimwengu kwamba ubongo wa mwanadamu ukilishwa chakula bora na ukaaminishwa kuamini vilivyo chanya, utakuwa hivyo na utajilazimisha kuwa hivyo siku zote za imani hiyo. Maneno yanaumba.

Uliwahi kukisikia kisa cha kitoto cha Malimi Busungu? Busungu alisajiliwa na Yanga akiaminika kwamba atakuwa akiwapa changamoto kina Donald Ngoma na Amissi Tambwe kwenye kikosi cha Hans van Pluijm wakati huo, kuongeza upana wa kikosi au kuchukua nafasi ya mmoja wapo endapo atakosa mchezo kwa sababu mbalimbali.

Ni wakati huo pia ambao angeweza kumshawishi Pluijm kumtumia kwenye michezo kutokana na aina ya mchezo au mpinzani aliyepo mbele yao.

Wakati akisajiliwa, alijua fika kwamba eneo alilotakiwa kucheza lilikuwa na ushindani mkubwa wa namba hasa kutokana na watu waliopo kufanya kazi ambayo hata yule mzee Cheka, baba yake Francis Cheka licha ya kuwa kipofu lakini aliiona kazi yao kwa kutumia macho ya masikio yake.

Mbali na hivyo, bado eneo hilo lilikuwa na watu wengi kama, Matheo Anthony, Paul Nonga ambaye aliamua kuondoka kwenda Mwadui, Busungu mwenyewe, Tambwe na Ngoma waliojijengea ngome yao. Je, ni kweli Busungu alitarajia mteremko hapo?

Ndiyo maana nikaanza na maneno ya mwanafalsafa Don Harvey, akili ya Busungu ilipokea na kuamini kwamba Hans Pluijm anamchukia, bila aibu akaja mbele yetu na kutuambia upuuzi huo, huwa najiuliza huyu Busungu achukiwe na Pluijm kwa kipi hasa? Pluijm analihitaji nini kutoka kwa Busungu?

Hii ndiyo aina ya wachezaji tulionao, mbaya zaidi akaamua kususa, hawa ndiyo wachezaji wa Tanzania ambao tunawategemea siku moja waifanye Tanzania ishiriki Kombe la Dunia.

Tatizo si hilo alilotuambia Busungu kipindi kile, alitudanganya na alitufanya watoto wadogo! Tatizo lake ni kutotulia na kucheza mpira, tatizo ni kutaka kupangwa bila kuonesha kiwango cha kuweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza.

Unawezaje kumshawishi Pluijm amweke benchi Tambwe kwa ajili ya mtu ambaye ndani ya robo tatu ya mwisho ya adui anapiga mpira bila malengo? Mtu ambaye siku zote hawezi kukuahidi kupata mabao wala kumchezesha straika mwenzake? Nadhani Tanzania itakushangaa na Jangwani yote itakuzomea.

Lakini maisha yamekwenda sasa, Pluijm hayupo tena kwenye benchi la Yanga, George Lwandamina ndiye bosi mpya wa Malimi Busungu, natamani nishuhudie kuona ule usahihi wa Busungu kuchukiwa na Pluijm! Natamani nione Busungu atamshawishi Lwandamina kumweka benchi Ngoma kwa ajili yake?

Busungu ili tukuamini kwamba akili yako haikuwa ya kitoto, unahitaji kuyaaminisha macho yetu kwa kukuona ukianza kwenye kikosi cha kwanza.

Busungu maneno huwa yanaumba, ulichokisema kwa Pluijm kiliumba kitu kwenye ubongo wako, mbaya zaidi kitu kilichoumbwa hakikuwa chenye uhalisia bali kilitengeneza ubongo wako ushindwe kuiamuru miguu yako kufanya kitu sahihi uwanjani.

Ninaamini miguu yako ina uwezo wa kufunga na kuisaidia timu yako. Ninaamini kwamba bado hujailisha akili yako chakula kinachostahili, ngoja nikwambie!

Maisha ya mchezaji yeyote yule yamezungukwa na misingi ya mchezo husika, ili mchezaji awe kwenye kiwango cha juu kila siku, ni lazima awe anaugusa mpira kutokana na eneo analocheza mara 1000 kwa siku. Huu ni utafiti wa kisayansi!

Kwa eneo analocheza Malimi Busungu, ili awe bora ni lazima apige mashuti 1000 kwa siku kuelekea langoni, hii ni nje na programu ya kocha wake.

Kama anahitajika mazoezini saa mbili asubuhi, ninatarajia kumuona Malimi Busungu akiamka mapema asubuhi na kuanza kufanya mazoezi yake binafsi ili kutimiza idadi ya kuugusa mpira mara 1000 ndani ya siku moja na baada ya hapo aendelee na programu ya George Lwandamina.

Nilitarajia kuona hata baada ya mazoezi ya Lwandamina, akifanya pia mazoezi yake binafsi na si kuja mbele yetu bila aibu usoni mwake kutuambia Pluijm alimchukia, Busungu ipo siku utatakiwa kula haya maneno yako, ipo siku utatakiwa kumuomba radhi kocha ‘profeshino’ kama yule.

Hivi sasa natarajia kukuona ukipambana kuingia kwenye kikosi cha kwanza, hapa nitakuelewa, lakini unaishi maisha sahihi kama mchezaji wa kulipwa?

Gazeti hili limekuwa likiwahoji wachezaji aina ya chakula wanachopendelea, huwa napigwa na bumbuwazi ninasoma mchezaji anasema anakunywa chai ya rangi na chapati mbili au chipsi wakati wa usiku. Sijapata fursa ya kuona chakula anachokula Busungu, lakini ili uweze kupambana na mikikimikiki ya walinzi wa aina ya Aggrey Morris au Jjuuko Murshid ni lazima uwe na stamina.

Mazoezi ya wanasoka ni magumu mno, unahitaji mlo kamili ‘balanced diet’ ili mwili uwe na nishati ya kutosha, Busungu kabla hujaona neema imekuja na ujio wa Lwandamina unapaswa ujiulize kwamba, unakula mlo kamili? Busungu maneno yanaumba!

Wewe si mchezaji usiyeweza kuishi maisha halisi ya soka, ni kutotulia kwako tu kisaikolojia ndiko kunakokufanya uishi kama unavyoishi, ni kutokupevuka kwako kimchezo ndiko kunaoondoka na ubora wako, mimi hali hii huiita mapepe.

Huwa najiuliza kwanini jiwe lisiwe dhahabu? Kwanini jiwe halikupewa thamani ya dhahabu? Jiwe na mapepe yake ndiyo chanzo cha kutokuwa dhahabu, ndiyo chanzo cha kutokuwa na thamani kama ilivyo kwa dhahabu, ninaamini siku ambayo jiwe litatulia na kuacha mapepe, litakuwa kama dhahabu na litapewa thamani sawa na dhahabu.

Mfumo wanaocheza Yanga unahitaji straika makini kule mbele, 4-4-2 huwa inaviungo wawili tu wa kati huku ikiwa na winga wawili, kwenye ligi tuliwashuhudia Niyonzima na Thabani Kamusoko, huku winga wakiwa na majukumu ya kucheza pembeni mno.

Hapa unapokutana na timu inayocheza na viungo zaidi ya wawili wa kati, huwazidi viungo hawa kwa kuwa huwa na uwazi kutoka kwenye winga mmoja kuingia ndani kumtafuta kiungo wa kati. Yaani kutoka kwa Simon Msuva au Deus Kaseke kuingia kwa Haruna Niyonzima. Hii ni 4-4-2 ‘flat’ siyo ‘diamond shape’.

Ili kutengeneza uwiano wa timu kimchezo, ni lazima straika namba mbili anayecheza nyuma ya straika namba moja ashuke kidogo chini kumsaidia kiungo mshambuliaji kukusanya mipira na kuanzisha mashambulizi.

Najaribu kuwaza ni eneo lipi ambalo Busungu huyu wa sasa anaweza kufiti na kuisaidia Yanga kwenye michezo migumu? Busungu huyu asiyeyajua majukumu yake, sioni akiisaidia Yanga akiwa kama straika namba moja au namba mbili.

Unapokuwa straika namba moja kwenye 4-4-2 tunataraji kuona ukifunga, unapokuwa straika namba mbili huwa na jukumu la kumchezesha straika namba moja pia kufunga unapopata nafasi.

Ni juhudi pekee itakayomfanya Busungu aweze kuendana na falsafa ya Yanga, ni nidhamu tu iliyoshikilia uwezo wake na ni kuiruhusu akili yake pekee kutulia na kuwa mtulivu ndicho kitakachomfanya awe mwenye thamani ya dhahabu.

Busungu si wewe tu ukitulia utakuwa na thamani kubwa sokoni, hata jiwe likiacha mapepe linaweza kuwa dhahabu siku moja.

Ushauri pekee unaoweza kuupata kutoka kwa mtu asiyesahihi ni ushauri usio sahihi, ninaamini bado nyota wetu wanahitaji kushauriana kupambana ili wafike kimataifa na si kushauriana kugomea mchezo.

Nakumbuka Hassan Isihaka alivyomgomea Jackson Mayanja, najaribu kuwaza Isihaka yuko wapi hii leo na Mayanja yuko wapi? Tumia kipaji ulichonacho. Miti huwa kimya pale ambapo hakuna ndege aimbaye isipokuwa ile tu ambayo ndege huimba vizuri. Busungu maneno huumba.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Katwila: Sitaidharau Mbeya City

NA VICTORIA GODFREY KOCHA wa timu ya Ihefu, Zuberi Katwila, amesema hawaraidharau  Mbeya City...

Kocha apokea kipigo kwa shingo upande

 NA  VICTORIA GODFREY KOCHA wa timu ya Mwadui, Khalid Adam, amesema amesikitishwa na kipigo cha mabao 6-1 kutoka kwa...

KMC kumaliza hasira kwa Gwambina

NA WINFRIDA MTOI BAADA ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga, kocha msaidizi wa timu ya Manispaa...

Tshishimbi atambulishwa kuvaa uzi wa AS Vita

NA MWENDISHI WETU KIUNGO wa zamani wa timu ya  Yanga, Papy Tshishimbi, ametambulishwa katika kikosi cha AS Vita ya...

Kaseja: Hatukuwa dhaifu kwa Yanga

NA ZAINAB IDDY NAHODHA wa timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC),  amesema  hawakuwa dhaifu mbele ya Yanga, licha ya...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -