NA SALMA MPELI,
NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesema kuelekea mechi yao dhidi ya JKT Ruvu, inayotarajiwa kupigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Uhuru, wanajipanga kuhakikisha wanachukua pointi tatu nyingine ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.
Akizungumza na BINGWA jana, wakiwa njiani kurejea Dar es Salaa wakitokea mkoani Kagera, Cannavaro alisema, Ligi ni ngumu na kila timu imejiandaa, lakini wao hawaangalii mtu, kwani kila timu itakayokuja mbele yao ni kichapo tu.
Alisema, hiyo inawasaidia kujiongezea pointi na kuzidi kuweka mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao msimu huu.
“Ligi ni ngumu na kila timu imejiandaa, lakini kwa upande wetu hatuangalii mtu, bali ni kuhitaji pointi tatu katika kila mechi iliyopo mbele yetu,” alisema.
Akizungumzia watani wao wa jadi, Simba, wanaoonekana kuhitaji ubingwa huo msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu minne, Cannavaro alisema, licha ya kuonekana wapo vizuri, lakini hilo haliwatishi, kwani wao wanaangalia mechi zao na nani wanacheza naye.
“Simba wanacheza mechi zao na sisi tunacheza mechi zetu, ushindi wao na kuwa kwao vizuri msimu huu haitutishi, kwani sisi tunahitaji kutetea ubingwa wetu, hivyo tunaangalia ya kwetu tu,” alisema.
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na pointi 21 na michezo 10 waliyocheza wakiwa na kiporo mechi moja dhidi ya JKT Ruvu, nyuma ya wapinzani wao Simba, wenye pointi 26 na michezo 10 waliyocheza kabla ya mechi ya jana dhidi ya Toto Africans ya Mwanza.