TIMU ya Mkoa wa Morogoro ya Netiboli imechukua ubingwa wa mashindano ya Kombe la Taifa ‘Taifa Cup’, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Morogoro wamechukua ubingwa huo baada ya kuwafunga wenyeji wa mashindano hayo mabao 38-33 katika mchezo wa fainali uliochezwa juzi mkoani humo.
Mashindano ya Kombe la Taifa tunayoona ni makubwa kwa Tanzania Bara kuwa yanatengeneza wachezaji wa kuunda timu ya taifa ya baadaye ambayo itashiriki mashindano ya kimataifa.
Kutokana na hilo, tulitegemea kwamba mikoa mingi ingejitokeza kushiriki mashindano hayo ili kuleta ushindani, lakini ni kutoa fursa kwa wachezaji kuonyesha vipaji vyao.
Pamoja na changamoto tuliyoiona katika mashindano hayo, sisi BINGWA tunaupongeza uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kwa kufanikisha kuandaa kombe hilo.
Tunasema kwamba tuna kila sababu ya kuupongeza uongozi ya Chaneta kutokana na mazingira magumu yaliyowezesha kukamilisha kalenda yao ya matukio ya mwaka mzima wa 2016.
Tunaamini kwamba uongozi wa chama hicho umefanya lile ambalo lingeweza kufanywa na vyama vingine vya michezo ambavyo vimeishia kumaliza mwaka bila kuandaa mashindano yoyote.
Pamoja na kujitokeza timu chache katika mashindano hayo, lakini vipaji chipukizi vimeonekana kwa timu za mikoa zilizopeleka wachezaji mjini Dodoma kushiriki Kombe la Taifa.
Tunasema kwamba, Chaneta wamethubutu licha ya changamoto ambazo walikumbana nazo katika kuandaa Kombe la Taifa, tunaamini kwamba wachezaji chipukizi walionyesha uwezo wa hali ya juu watapata nafasi kwenye timu ya taifa ya baadaye.
Tunaamini kwamba wachezaji hao watakuwa tegemeo kwa timu ya taifa na Chaneta kwa kushirikiana na mikoa wanatakiwa kulinda vipaji vyao.
Tunamaliza kwa kusisitiza kwamba viongozi wa vyama vya michezo wanatakiwa kuiga mfano wa Chaneta wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa kuzingatia matukio ya kalenda ya mwaka mzima ya mashindano ili kuinua michezo nchini.