Tuesday, October 20, 2020

DAR DERBY, ATAKAYEKISHINDA CHUMBA CHAKE ATASHINDA VITA YOTE

Must Read

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu...

NA HALIDI MTUMBUKA,

NI vita ya kasi ya Shiza Kichuya na utayari wa mwili wa Mwinyi Haji, ni vita ya nguvu za Andrew Vincent ‘Dante’ na akili za Ibrahim Ajib, ni vita ya mikono ya Vincent Angban dhidi ya kichwa cha Amissi Tambwe, ni vita ya Donald Ngoma dhidi ya Method Mwanjali, ni vita ya Laudit Mavugo na Kelvin Yondani. Hii ni vita ya kimwili na kiakili, kimbinu na kiufundi. Tayari imeshapiganwa ndani ya mioyo yetu na tayari tumeshampata mshindi kwenye fikra zetu, zimebaki dakika tisini zenye maana moja tu kati ya nyingi zijulikanazo, nayo ni kumpata mshindi atakayezawadiwa pointi tatu. Hizi ni dakika tisini ambazo ushindi pekee huwa ndio wenye maana kwa kila mmoja, si Hans Van Pluijm wala Joseph Omog, si mzee Akilimali wala Zackaria Hanspope, wote wanaota ndoto zinazofanana, wote mioyo yao inadunda kwa kasi hivi sasa, wanahitaji pointi tatu. Ndiyo maana nikaiita vita, lakini si vita yenye uhalisia wa vita bali ni vita yenye maana ya mchezo wa kiuungwana ambao hauna madhara kwa binadamu. Hebu tuuangalie mchezo wenyewe!

Tangu ligi ianze Simba imeshacheza michezo sita, ikashinda michezo mitano ambayo ni sawa na asilimia 83.3 za ushindi kwenye michezo hiyo, imetoa sare mchezo mmoja ambao ni sawa na asilimia 16.7 za michezo yote huku ikiwa haijafungwa mchezo hata mmoja, nayo ni sawa na asilimia 00.00.

Yanga imeshuka dimbani kwenye michezo mitano, ikashinda michezo mitatu ambayo ni sawa na asilimia 60 za ushindi kwenye michezo yote, sare mchezo mmoja ambao ni sawa na asilimia 20 huku ikifungwa mchezo mmoja ambao ni sawa na asilimia 20.

Simba inaingia kwenye vita hii huku wanajeshi wake wakiwa kwenye morali kubwa ya ushindi wakichagizwa na asilimia sifuri ya kutopoteza mchezo wowote wa ligi kuu msimu huu, Yanga inaingia vitani huku wanajeshi wake wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kupoteza mchezo mmoja tena wa mwisho kabla ya kuivaa Simba, kiuhalisia kupoteza mchezo hukipunguzia kikosi ari ya upambanaji. Inaweza isiwe sahihi sana endapo utakuwa na wimbi la wachezaji waliopevuka kimchezo na wenye uwezo wa kuendana na mazingira hasi mchezoni, yaani kupoteza ni sehemu ya mchezo wenyewe.

Wachezaji wafuatao ni wageni kabisa katika mpambano huo wa kihistoria uliodumu mjini kwa takribani miongo minane, Simba ni Jamali Mnyate, Shiza Kichuya, Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon, Janvier Bokungu, Method Mwanjali, Mohamed Ibrahim, Mzamiru Yassin, Malika Ndeule, Hamadi Juma, Mussa Ndusha na Amme Ally. Yanga ni Beno Kakolanya, Andrew Vicent, Obrey Chirwa, Juma Mahadhi na Yusufu Mhilu.

Orodha ya wachezaji wageni kabisa kwenye vita hii kwa upande wa Simba inaonekana kuwa kubwa kulinganisha na upande wa Yanga, uhalisia wake ni kwamba kikosi cha Yanga kina muunganiko wa wachezaji waliodumu tangu msimu uliopita na wanalifahamu fika joto la vita yenyewe, wengine walishawahi kukabidhiwa bendera ya vita yenyewe na hawahitaji kusimuliwa chochote, hii ni faida kwa Yanga kwa kuwa siku zote uzoefu ndio mwalimu bora, tofauti na Simba ambayo itakuwa ikikumbana na changamoto ya baadhi ya wanajeshi wake kukosa uzoefu wa uwanjani na hapo pia itategemea na saikolojia zao na namna walivyopevuka kukabiliana na michezo yenye presha kubwa kama hii. Unahitaji kuuzuia moyo wako dhidi ya mihemko ya nje ya uwanja ili kupambana kwenye mchezo huu. Kuna namna ambavyo hawa wageni pia watahitaji kuonesha kwanini wanastahili kuwepo walipo.

Ubora wa kikosi cha Simba huanzia kwenye umiliki wa mpira, wanachokifanya huwa ni kujitahidi kuuficha mpira na kuuweka katika utawala wao, hapa ndipo Jonas Mkude ambaye amezaliwa upya akiwa juu ya Mwanjali na Jjuuko au Lufunga huwa ni muhimu kwenye ulinzi na mipira iliyoshindikana hutulizwa kwenye umiliki wake kisha hupiga pasi zinazoituliza Simba kwenye eneo la kiungo, huu ndiyo moyo wa Simba na hapa ndipo zilipochemba zote nne na mirija yote inayosambaza damu kwenye eneo lote la timu ya Simba.

Yanga wanatakiwa waanze kuvuruga mapigo ya moyo wa Simba kwanza kisha ndiyo waanzishe zile ndoto zao wanazoziota hivi sasa, wanahitaji kuzuia utendaji kazi wa Mkude kwenye utawala wake ili kina Jamal Mnyate washindwe kusambaziwa mipira kwa wakati sahihi hatimaye Ibrahim Ajib awe anazurura tu mbele ya Dante. Hivyo hivyo kwa Kichuya na Mavugo.

Yanga wamekuwa na muunganiko bora wa kikosi kutokana na kuelewana kwao kwa muda mrefu, lakini unawezaje kuuacha ubora wa utumiaji wa nafasi wazipatazo kuhakikisha wanafunga mabao? Kwenye michezo miwili, ule dhidi ya Majimaji walipiga mashuti sita yaliyolenga lango, wakafunga mabao matatu dhidi ya African Lyon, walipiga saba yaliyolenga lango na kufunga mabao matatu.

Ubora huu unachagizwa na jinsi ambavyo Donald Ngoma amekuwa na uwezo wa kutulia na mpira kwa muda mrefu mbele ya mabeki wa wapinzani, ni hapo pia mawinga wa Yanga hutumia mbinu ya kutozoeleka kwa kubadilishana upande huku wakitumia kasi zao. Kuna mtu hatajwi sana, haonekani sana uwanjani lakini ni hatari sana, huyu ni Amissi Tambwe ambaye ukimsahau hutumia muda huo kukukumbusha uwepo wake dimbani. Vichwa vyake vitaingia kwenye vita kali dhidi ya mikono ya Angban.

Kwa upande wa Simba endapo watahitaji ushindi kwenye mchezo huo, wanahitaji kwanza kukataa presha kwa wanajeshi wake wageni kisha kule mbele kunahitajika awepo straika namba moja na namba mbili. Mfumo huanza kumuonesha Mavugo kuwa ndiye straika namba moja huku Ajib akiwa ni namba mbili, cha ajabu wakati mchezo ukiendelea hakuna anayefanya shughuli yake, wote huhitaji kufunga tu na ni bora Ajib akasimama nyuma ya Mavugo ili kumchezesha au aanzie benchi kuusoma mchezo na Blagnon aanze kwa kuwa pia anaweza kukaa na mpira kwa sekunde kadhaa tofauti na wawili hao. Kisha Ajib atumike kama silaha ya akiba pale itakapohitajika ili kumpunguzia uwezekano wa kupata kadi. Kasi ya Shiza Kichuya na muunganiko wa wawili hao ukipata huduma sahihi kutoka kwenye eneo la kiungo huenda ukasumbua sana ngome ya ulinzi ya Yanga ambayo hairuhusu mabao mengi mbele ya Vincent Bossou.

Endapo utahitaji kilicho bora kutoka kwa Mavugo, ni lazima awe huru uwanjani kufanya anachotaka na si kumpangia majukumu maalumu yatakayomfanya aone jukumu lote la kuhakikisha Simba inapata mabao lipo mabegani mwake, yaani kwa lugha nyepesi ni kama ambavyo Donald Ngoma hucheza kwenye kikosi cha Yanga.

Kwa ujumla mchezo hautarajiwi kuwa tofauti sana na michezo mingine iliyotangulia dhidi yao. Vita hii itapiganwa kwa nidhamu ile ile, yaani nje ya uwanja kutakuwa kunahusika sana kutokana na kuhusika kutengeneza presha kwa wachezaji na makocha, mchezo hautakuwa tofauti na jinsi ambavyo makocha wa timu zote wataziandaa timu zao kwenye vyumba vya kubadilishia nguo. Atakayefanikiwa kukiteka chumba chake ndiye atakayekuwa amefanikiwa kuishinda vita, unahitaji pia uwezo wa kimbinu na kiakili kwa wachezaji wako ili kupambana.

Lakini pia utumiaji wa nafasi, upangaji wa mashambulizi na upanguaji wa ngome za ulinzi utaamua mchezo huu.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya wanamuziki wa Tanzania ambao miongoni...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara  (VPL), utakaochezwa leo...

Mugalu atema cheche Simba

NA ASHA KIGUNDULA MSHAMBULIAJI wa Simba, Chris Mugalu, amesema wanakwenda mkoani Rukwa kupambana na kupata ushindi katika mchezo wao...

Malale aitisha Yanga

NA ZAINAB IDDY KOCHA Mkuu wa timu ya Polisi Tanzania, Malale Hamsini, amezisikia sifa za kocha mpya wa Yanga,...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -