Tuesday, October 20, 2020

DE JONG ANAMFANYA CRUYFF ATABASAMU HUKO ALIKO

Must Read

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu...

GWIJI la Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Johan Cruyff, enzi za uhai wake aliwahi kusema: Mchezo wa soka ni mwepesi kuucheza lakini hakuna kitu kigumu kama kucheza soka jepesi.

Wapo wengi walioishi katika msemo huo wa Cruyff.

Mfano kwa miaka mingi sasa timu ya Barcelona inaishi kwenye msemo wa mwasisi huyo wa ‘Tiki-Taka’, Cruyff.

Kuanzia Barca ya mwanafunzi mtiifu wa Cruyff, Pep Guardiola hadi ya hivi sasa bado inaendelea kucheza hivyo, hata Mhispania huyo alipokwenda Bayern na sasa Man City, anaendeleza imani hiyo ya kuufanya mchezo wa soka uwe mwepesi zaidi.

Kwa wachezaji, naomba leo nimchambue huyu dogo wa Ajax, timu ambayo Cruyff aliwahi kuichezea.

Dogo anaitwa Frenkie De Jong. Tayari ameshatabiriwa kuwa mchezaji bora zaidi ya wachezaji wakubwa na wenye heshima zao kama vile Franz Beckenbauer.

Usishtuke sana, ni uwezo wake mkubwa wa kuuchezea mpira, bila presha, bila kutumia nguvu nyingi, matumizi makubwa ya akili ndivyo vimemfanya atikise kwa sasa.

Dogo huyu ni kama anaelea kwenye pepo ya soka. Na zaidi ya hilo, anamfanya Cruyff atabasamu huko aliko, kwa sababu anaufanya mchezo wa soka uwe mwepesi mno.

Pengine kuanza kumfananisha na Beckenbauer au hata Sergio Busquets ni suala la mapema sana kwa kijana huyu mwenye umri wa miaka 21.

Lakini hebu jiulize, ni wachezaji wangapi waliochipukia miaka ya hivi karibuni uliwasikia wakifananishwa na Lionel Messi?

Je, walifikia kiwango chake au walibaki kuwa wachezaji wa kawaida kuliko neno lenyewe, kawaida.

De Jong ana haki ya kusajiliwa na timu yoyote kubwa kwa sasa. Ana haki ya kufananishwa na kiungo yeyote yule wa zamani mwenye ubora kama wake.

Mtazame alivyo, ana sura ya kitoto. Na kweli, kiumri bado ni mdogo sana, miaka 21 imeshakatika tangu alipozaliwa lakini kila anapokuwa na mpira mguuni, huwa anafikiria vitu viwili.

Namna ya kuipunguzia presha safu yake ya kiungo na ya ulinzi, lakini pia muda gani na katika nafasi gani apige pasi ya uhakika.

Vyote hivyo vinafanywa na ubongo wa kijana huyo wa Ajax ambaye kiasili ni kiungo wa kati, lakini akiwa na uwezo mwingine mzuri sana wa kiufundi wa kucheza katikati ya mabeki wawili wa kati.

Huyo ndiye De Jong. Haishangazi sana kusikia jina lake likitikisa katika ulimwengu wa soka kwa sababu uwezo wake nao si wa kawaida.

Nieleweke vizuri hapa, sijazidisha chumvi katika neno lolote.

Andiko hili na mengine yote utakayokutana nayo kumhusu De Jong ni ya kweli kabisa. Ni sawa na yaliyozungumzwa kuhusu wachezaji waliochipukia na kuishangaza dunia.

Wapo walioibuka na kupotea. Kundi hili wapo Mikel Oyarzabal wa Real Sociedad na Tammy Abraham wa Chelsea. Kwa uchache.

Pia walioibuka, wakapotea na kurudi tena kwenye ramani. Kundi hili utawapata nyota kama vile Renato Sanches wa Bayern na Goncalo Guedes wa Valencia. Nao kwa uchache.

Kuna wale ambao wameibuka hivi sasa na tunaendelea kuangalia maendeleo yao. Hapa wapo Malcom wa Barcelona, Carlos Soler wa Valencia, kuna Ruben Neves wa Wolves na kijana wetu wa Afrika, Franck Kessie anakipiga AC Milan.

Halafu kuna hili kundi ambalo limejaa vijana wenye uwezo mzuri mno duniani kwa sasa. Andreas Christensen wa Chelsea, Marco Asensio pale Real Madrid, Ousmane Dembele (Barcelona), Dele Alli (Tottenham) bila kumsahau Kylian Mbappe wa PSG.

Hao ni wachache kati ya wengi. Kuna waliofananishwa na Messi humo, wengine walipewa cheo cha Pele, Maradona, Andy Cole. Na wengineo.

Lakini ni wangapi wanasubiri kuuona uwezo wa De Jong katika ligi kubwa zaidi ya Eredivisie pale Uholanzi?

Wangapi wanataka kushuhudia miguu ya De Jong ikiyafanya yale ambayo yalisemwa yatakuwa makubwa zaidi ya Beckenbauer na Busquets?

Bila shaka wapo wengi sana. Ni suala la muda tu hadi dogo huyo atakaposajiliwa na moja ya miamba ya soka duniani ili aweze kufanya yote ambayo yanasubiriwa.

Tetesi za usajili zinamhusisha sana na Barcelona, Real Madrid, Tottenham na Man City. Zote hizo ni timu zinazofaa kuwa na mchezaji mwenye ubora kama wa De Jong.

Barcelona inataka kuwekeza kwa De Jong kwa sababu Busquets atafikia wakati hataweza tena kuendana na kasi ya soka la kisasa linalozidi kuchanua kwa mbinu tofauti tofauti.

Vipi kwa upande wa Man City. Si unakumbuka Pep Guardiola alitaka kumsajili Jorginho akamkosa? Sababu haikuwa ngumu sana kuing’amua, umri wa Fernandinho.

Mbrazili huyo kwa sasa ana miaka 33. Ni kamari mbaya sana kwa upande wa Man City kuendelea kumtumia kiungo mkabaji mwenye umri mkubwa kiasi hicho. Salama yao ni kwamba Fernandinho anazeeka na utamu wake.

Mfano wa hizo timu mbili unadhihirisha jinsi gani ubora wa De Jong ulivyo. Ni kama keki tamu inayosakwa kila kona.

Mchawi pekee kwake ni uzoefu tu lakini kwangu mimi naamini hilo halizuii yeye kucheza soka Ligi Kuu za Hispania na England.

Nadhani ukiachana na kule Hispania ambako Real Madrid na Barcelona zina nguvu zaidi ya kumchukua huyu dogo, sehemu nyingine ambayo De Jong anasubiriwa kwa hamu ni England.

Kuna timu mojawapo pale inamtosha De Jong. Kuna sehemu ya historia inamsubiri pale England.

Historia ambayo Cristiano Ronaldo na Eden Hazard wanaimiliki. Hao ndio wachezaji pekee ninaokumbuka ambao walitoka ligi zenye ubora hafifu na kuiteka England.

Na zaidi, ili aweze kuendelea kuifanya sura ya Cruyff itabasamu.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya wanamuziki wa Tanzania ambao miongoni...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara  (VPL), utakaochezwa leo...

Mugalu atema cheche Simba

NA ASHA KIGUNDULA MSHAMBULIAJI wa Simba, Chris Mugalu, amesema wanakwenda mkoani Rukwa kupambana na kupata ushindi katika mchezo wao...

Malale aitisha Yanga

NA ZAINAB IDDY KOCHA Mkuu wa timu ya Polisi Tanzania, Malale Hamsini, amezisikia sifa za kocha mpya wa Yanga,...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -