NA ZAITUNI KIBWANA,
MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul ‘Diamond’, ameonekana kuchanganyikiwa na ujauzito wa mpenzi wake, Zarinah Hassan ‘Zari Boss Lady’, baada ya msanii huyo kummwagia sifa kila kukicha.
Diamond ambaye ametoa wimbo mpya jana unaojulikana kwa jina la Maria Salome, kwenye ukurasa wake wa Instagram amekuwa akiweka picha za mrembo huyo kutoka Uganda na kummwagia sifa kedekede.
Kwenye ukurasa huo, Diamond aliweka picha ya Zari ikimuonyesha vema jinsi tumbo lake lilivyo kwa sasa na kuandika: “Mwanamke mjamzito siku zote anavutia, Damn! Kama nitokee hapo.”
Ujumbe huo umewafanya mashabiki wake kumpongeza msanii huyo kwa kutarajia kuitwa baba kwa mara nyingine.
Zari tayari amemzalia Diamond mtoto mmoja wa kike anayejulikana kwa jina la Latifa maarufu kama Tiffa, ambapo kwa sasa anatarajia mtoto wa kiume.