LONDON, England
MKONGWE wa zamani wa timu ya taifa ya Senegal, El Hadji Diouf, amesema mabeki Joel Matip na Allan Nyom, watayajutia maamuzi yao ya kutoitumikia timu yao ya taifa ya Cameroon kwenye Fainali za Mataifa Afrika (Afcon 2017) ambayo ilifikia tamati usiku wa kuamkia leo.
Cameroon ilitarajiwa kukutana na Misri kwenye fainali licha ya takribani wachezaji nane kugoma kutoitikia wito wa kocha wao, Hugo Broos.
“Sielewi kwanini watu wanazigomea timu zao za taifa,” alisema Diouf alipokuwa akihojiwa na kituo cha matangazo cha BBC.
“Mkongwe wa reggae, Bob Marley, alikuwa akisema kila siku, ‘kama hujui ulipotoka, hutajua mahali unakokwenda,” aliongeza.
“Kuwa Mwafrika ni jambo gumu, kwa sababu hata ukiwa kocha bora kutoka huku hawatakupa PSG, Barcelona, Liverpool au Manchester United uzifundishe.
“Ndio maana ninawaambia hawa vijana: Msizikatae timu zenu za taifa kwani hii dunia yote itabebwa na Africa,” alisema.