ISTANBUL, Uturuki
MOJA ya matukio ya kusikitisha yaliyowahi kumkuta mshambuliaji wa zamani wa Barcelona, Samuel Eto’o, ni ya ubaguzi na sasa klabu yake ya Antalyaspor inayoshikiri Ligi Kuu ya Uturuki imemwondoa kwenye kikosi cha kwanza mpaka pale maelezo ya kina kuhusu malalamiko yake ya ubaguzi yatakapotolewa.
Eto’o, ambaye pia ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii ‘Instagram’ akisema: “Labda watu hawaniheshimu kwa sababu mimi ni mtu mweusi.”
Lakini baada ya viongozi wa klabu kuuona ujumbe huo, Eto’o aliandika ujumbe wa pili akijitetea kwamba hakumlenga Mwenyekiti wa Antalyaspor, Ali Safak Ozturk katika ujumbe wake wa kwanza.
“Ujumbe wangu ulikuwa kwa mtu yeyote anayenikosoa kwa miaka mingi, lakini mimi niliendelea kunyakua mataji,” ulisomeka ujumbe huo wa kujitetea wa Eto’o.
Hivi karibuni, Ozturk alimkosoa Eto’o kwa kiwango dhaifu alichokionyesha mwanzoni wa msimu huu na alinukuliwa akisema: “Hakuna mchezaji aliyeko juu ya matakwa ya Antalyaspor, kila mmoja ajue nafasi yake.”
Klabu hiyo ilisema kuwa Eto’o atakuwa na mazoezi ya peke yake mpaka pale kesi yake itakapojadiliwa na bodi ya klabu.
Antalyaspor wako kwenye wakati mgumu baada ya kuanza msimu huu vibaya na kuambulia pointi moja katika mechi nne walizocheza hadi sasa.