Tuesday, October 27, 2020

FAINALI MISS TANZANIA 2016 LEO…

Must Read

Boni Mwaitege amkalisha Mgogo

NA VALERY KIYUNGU KUPITIA shindano la Nani Zaidi linaloendeshwa na redio Passion Fm ya...

Mzuka warudi tena kwa s2kizzy

NA CHRISTOPHER MSEKENA SIKU chache baada ya kuvamiwa na kufanyiwa uharibifu wa studio zake...

The Yeamen waipiga ‘Shoti’

NA JEREMIA ERNEST MSANII kutoka kundi la The Yeamen, Suma Toto, amewaomba mashabiki wa...
  • Dar kukiona cha moto kwa Iringa, Singida, Mwanza
  • Hashim Lundenga atoa neno zito, warembo roho kwatu Mwanza

NA MICHAEL MAURUS

FAINALI za mashindano ya urembo nchini ya Miss Tanzania, zinatarajiwa kufanyika leo jijini Mwanza, pale warembo 30 watakapopanda jukwaani kuwania taji hilo linaloshikiliwa na mrembo kutoka Arusha, Lilian Kamanzima.

Kilele cha mashindano hayo makubwa ya urembo hapa nchini kwa mara ya kwanza kinafanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni moja ya mkakati wa waratibu wa tukio hilo, Kampuni ya Lino International Agency, chini ya ukurugenzi wa Hashim Lundenga ‘Uncle’, kupanua wigo wa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Lundenga, wameamua kuyatoa mashindano hayo nje ya Dar es Salaam ili kudhihirisha kwa vitendo kuwa shindano hilo ni la kitaifa na si la mkoa mmoja pekee.

“Kwa miaka yote fainali za mashindano yetu zimekuwa zikifanyika Dar es Salaam, katika hilo nikiri tuliteleza kidogo, japo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni kutokana na shinikizo la wadhamini ambao wamekuwa wakitoka Dar es Salaam.

“Lakini safari hii japo mdhamini mkuu yupo Dar es Salaam, tumeona ni vema tukahamia mikoani, ambapo Jiji la Mwanza ndilo lililopata bahati ya kufungua dimba na nadhani tutaendelea kutoa nafasi kwa mikoa mingine zaidi kuwa wenyeji wa mashindano haya,” anasema Lundenga.

Juu ya mwitikio wa wakazi wa Mwanza kwa shindano hilo kufanyika mkoani humo, anasema: “Tunashukuru tumepokewa vizuri na kila tulipokwenda wakazi wa hapa wameonyesha kuvutiwa mno na warembo na kuwa na shauku ya kufahamu iwapo taji litabaki hapa Mwanza au la.

“Ikumbukwe kuwa, Jiji la Mwanza lina historia nzuri katika mashindano haya, kwani limeshawahi kutwaa taji mara mbili mfululizo, mwaka 2009 ambapo mshindi alikuwa ni Nasreen Karim na mwaka 2010, Miriam Gerard.”

Anasema ni matarajio yao wataendelea kupata sapoti zaidi miaka ijayo katika mikoa watakayokuwa wakifanyia fainali hizo, kama ilivyokuwa jijini Mwanza.

Warembo 30 wanaowania taji hilo mwaka huu ni Julitha Kabethe (Dar City Centre), Nuru Kondo (Ukonga), Grace Malikita (Tabata) na Spora Luhende (Dar City Centre) kutoka Kanda ya Ilala.

Wengine ni Diana Edward (Ubungo), Regina Ndimbo (Dar Indian Ocean), Ndeonansia Pius (Sinza) na Hafsa Abdul (Sinza) kutoka Kanda ya Kinondoni; Mwantumu Ally (Mbagala), Esther Mnahi (Kigamboni) na Anitha Kisima (Mbagala), hiyo ikiwa na Kanda ya Temeke na Upendo Dickson (Lindi), Abella John (Morogoro), Elineema Chagula (Morogoro) pamoja na Irene Ndibalema (Mtwara).

Pia wapo Anna Nitwa (Dodoma), Lisa Mdolo (Singida) na Irene Massawe (Singida), Laura Kway (Chuo Kikuu cha Iringa), Iluminatha Dominic (Geita), Maria Peter (Mwanza) na Lucy Michael (Geita), Mourine Ayoub (Arusha), Glory Stephano (Kilimanjaro), Elgiver Mwasha (Tanga) na Bahati Mfinanga (Manyara).

Warembo wengine wanaotarajiwa kupanda jukwaani leo kuwania taji hilo na hatimaye kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Dunia, yaani Miss World, ni Mourine Komanya (Iringa), Anitha Mlay (Iringa), Irene Msabaha (Ruvuma) na Eunice Robert (Mbeya).

Wakizungumzia shindano la mwaka huu, warembo hao wamelielezea kutarajia kuwa la aina yake, zaidi ikiwa ni kutokana na kufanyika nje ya Dar es Salaam, lakini pia kile wanachoamini ubora wa washiriki, hivyo kufanya ushindani kuwa wa aina yake.

Akizungumza na BINGWA, mmoja wa warembo hao, Laura Kway, anasema: “Kwa kweli shindano la mwaka huu litakuwa na upinzani mkali, kwani warembo wote ni wazuri na wenye vigezo vinavyotakiwa, ila amini usiamini, unayeongea naye (yeye) ndiye Miss Tanzania 2016, kwani nina vigezo vyote vinavyohitajika katika mashindano haya, ninajiamini na sina shaka na taji kwenda Iringa University na kuweka rekodi ya mwanafunzi wa chuo kutwaa taji kwa mara ya kwanza.”

Kwa upande wake, Grace Malikita, alitamba: “Japo washiriki wenzangu nao ni warembo, lakini sioni wa kunizidi, nipo vizuri, ninajiamini na nimejiandaa kutwaa taji na kuendeleza ubabe wa Ilala kwa kutwaa mataji ya Miss Tanzania, nawaomba wakazi wa Ilala waniombee.”

Mrembo mwingine, Spora Luhende, alisema: “Kutokana na maandalizi niliyofanya tangu awali, sina shaka lazima nitatwaa taji la Miss Tanzania kwani nina vigezo vyote vinavyotakiwa, kuanzia uzuri wa sura, umbo, kujiamini na kujieleza pia.”

Naye Irene Massawe anasema: “Kwa kweli ushindani utakuwa mkali, kwani warembo wote ni wazuri, lakini nakuhakikishia taji la Miss Tanzania mwaka huu lazima litakwenda Singida.”

Kwa ujumla, fainali za mashindano ya mwaka huu, zinatarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani takribani washiriki wote wameonekana kuwa na vigezo vinavyotakiwa.

Ikumbukwe kuwa, mashindano hayo yanafanyika ikiwa ni baada ya kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa madai ya kukiuka taratibu za mashindano ya sanaa, kabla ya kufunguliwa likiwa limekaa ‘lupango’ kwa mwaka mmoja.

Baada ya kufunguliwa, wapo walioamini shindano hilo litapoteza mvuto na kukosa washiriki, lakini haikuwa hivyo, kwani warembo waliojitokeza ni wazuri mno kiasi kwamba wengine walikosa nafasi ya kutinga fainali, akiwamo Happiness Mushi, aliyeishia hatua ya Kanda ya Kinondoni.

BINGWA, lililopata bahati ya kuwa karibu na washiriki wa mwaka huu walipokuwa Dar es Salaam kabla ya kuhamia Mwanza, lilijionea jinsi ushindani utakavyokuwa mkubwa leo jijini Mwanza.

Na kati ya mikoa ambayo inaweza kuwa tishio kwa Dar es Salaam inayoongoza kutwaa taji la Miss Tanzania, kuna Iringa, Singida, Mwanza, Morogoro na mikoa mingineyo.

Hata hivyo, bado Dar es Salaam wana nafasi kubwa ya kutwaa taji kutokana na ubora wa baadhi ya warembo wake, hasa wale wa Ilala na Kinondoni ambao wameoneka kukamilika kila idara.

Mwisho wa siku, ni suala la kusubiri na kuona kama si kusikia kwamba ni mkoa gani utakaoibuka kidedea leo na kutwaa taji hilo kulitoa mikononi mwa mrembo wa Arusha, Lilian Kamanzima.

Akizungumza fainali hizo, Lundenga alisema: “Tumejiandaa vilivyo na wadau wa urembo na Watanzania kwa ujumla watarajie shoo ya kiwango cha kimataifa na tunaamini atapatikana mrembo bomba atakayeipeperusha vema Bendera ya Tanzania Miss World baadaye mwaka huu.”

Aliwataka wadau wa fani hiyo kuendelea kuwasapoti, huku akitoa onyo kali kwa wale wote ambao wamekuwa wakilifanyia ‘figisufigisu’ shindano hilo kutokana na chuki zao binafsi kwamba wasitarajie ushindi katika hilo, kwani wamejiimarisha kila kona kuepuka yaliyowakuta awali na kujikuta shindano hilo likifungiwa.

Fani ya urembo ni miongoni mwa sanaa ambayo imekuwa ikijizolea umaarufu duniani kote kadri siku zinavyozidi kwenda, japo kuna vipindi kadhaa, imekuwa ikipitia katika milima na mabonde.

Shindano la Miss World linaelezewa kuwa linashika nafasi ya tatu duniani kwa umaarufu, likitanguliwa na fainali za soka za Kombe la Dunia na michezo ya Olimpiki.

Kwa hapa nchini, mashindano ya urembo yalizinduliwa mwaka 1967, japo yalianza kupata umaarufu zaidi mwaka 1994, yalipoanza tena rasmi baada ya awali kuzuiliwa na serikali kwa madai kuwa yanakiuka maadili ya Kitanzania.

Hadi leo ambapo Tanzania inasubiri kumpata mrembo wake wa 23, shindano hilo limeendelea kuwa kimbilio la warembo nchini kutokana na ukweli kwamba, limekuwa likiwawezesha kutimiza ndoto zao katika fani ya urembo, lakini pia kuwapa fursa mbalimbali zinazowafanya kubadili maisha yao.

Kwa kawaida mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka, yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa fani hiyo na hata wale wasio mashabiki ambao kwa kiasi fulani wako tayari kusikia au kuona tu nani anakuwa Miss Tanzania mpya kisha waendelee na hamsini zao.

Hamasa ya shindano hilo imekuwa ikijengwa na mambo kadhaa kwa muda wote tangu mwaka 1994, pale mfumo wa patashika hiyo ulipoanza kuchukua sura mpya ya kiuchumi kwa washiriki na hasa washindi.

Ni mashindano ambayo yamekuwa yakipanda chati kila mwaka kutokana ukubwa wa zawadi zake, fursa za ajira kwa washiriki, hasa katika biashara ya mitindo na matangazo.

Kwa haraka, mashindano ya urembo yanachukua nafasi ya kwanza kwa kuwa na zawadi kubwa kwa washindi (mmoja mmoja), pengine kuliko mashindano yoyote ya michezo au hata sanaa hapa nchini.

Washindi wake wamekuwa wakizawadiwa magari, fedha kwa kiwango cha mamilioni na hata vifaa vingine vya thamani kubwa, ikiwamo nyumba iliyowahi kutolewa mara moja.

Hata hivyo, mashindano hayo yamekuwa pia yakipitia magumu kutokana na changamoto za kimaadili, kwa nyakati fulani kuonekana kama hayaendani na maadili, hasa katika suala la mavazi na tabia za warembo waliowahi kushiriki.

Hili si kwa Tanzania pekee, changamoto hii ipo pia katika nchi kadhaa duniani na kwa haraka dhana kubwa inayohusishwa hapo husababishwa na hisia au imani kuwa mashindano hayo huchochea biashara ya ngono.

Nakumbuka Novemba 30 mwaka 2007 nilipokuwa nchini China, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Miss World, Julia Morley, alithibitisha hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Crowne Plaza, kisiwani Sanya, ambako shindano la Dunia la mwaka huo lilikuwa likifanyika.

“Ninafahamu kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakichukulia mashindano yetu (kuanzia Miss Tanzania hadi Miss World) kama ni uhuni, lakini hilo si kweli, mwaka huu (2007) tumepanga makusudi fainali za shindano hili kufanyika Siku ya Ukimwi Duniani (Desemba Mosi) kama sehemu ya kuonyesha nasi tunapingana na tatizo hilo, tukihimiza kupiga vita Ukimwi na virusi vyake,” Julia alisema.

Historia ya shindano la Miss World inaanzia mwaka 1951, japo lilianza kutambulika rasmi kimataifa mwaka 1959, lilipoanza kuratibiwa na Eric Morley.

Hapa kwetu rekodi zinaonyesha tulianza mashindano hayo mwanzoni mwa miaka ya 1960, japo hayakuwa katika mfumo wa kitaifa zaidi na mrembo wa kwanza alipatikana mwaka 1967, akiwa ni Theresa Shayo.

Lakini baadaye shindano hilo lilikuja kupigwa marufuku na Serikali chini ya utawala wa TANU, kutokana na kuonekana kwenda kinyume na maadili. Hiyo ilikuwa mwaka 1967.

Mabadiliko ya kiuchumi yaliyotokea nchini wakati wa utawala wa awamu ya pili chini ya Serikali ya Alhaji Ali Hassan Mwinyi, yalichangia kubadilika kwa mfumo wa kijamii nchini, hivyo kutoa mazingira ya kurejea tena kwa mashindano hayo mwaka 1994.

Wazo la kurejea kwa mashindano hayo liliasisiwa na Hashimu Lundenga, aliyeamua kumshirikisha Prashant Patel, ambao kwa pamoja waliishirikisha hoteli ya White Sands ya jijini Dar es Salaam na kulirejesha shindano hilo.

Lakini kama ilivyo kawaida ya kitu chochote katika hatua za mwanzo, mwaka huo (1994) maandalizi yake hayakuwa ya kishindo na shindano lilishirikisha washiriki wachache wasio wa wigo sahihi kulingana na upana wa nchi.

Hata hivyo, mrembo Aina Maeda alifanikiwa kubeba taji mwaka huo na kupata tiketi ya kwenda Miss World.  Hatua ya Aina kwenda kwenye Shindano la Dunia na kutangazwa kwake kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari, ambavyo navyo ndiyo vilianza kuwa vingi kulingana na mabadiliko hayo, kulisaidia mno kuanza kukua kwa shindano hilo.

Ni kutokana na kukua kwa mvuto wake ndani ya jamii, taratibu makampuni na mashirika mbalimbali yalianza pia kujitumbukiza kwa njia ya udhamini, hali iliyoanza kuyaboresha hasa katika suala la zawadi.

Tangu kuanza kwa shindano hilo, mafanikio ya juu yalipatikana mwaka 2005, pale Nancy alipotwaa taji la Miss World Afrika, akiwa amefanikiwa kutinga hatua ya sita bora ya michuano hiyo iliyofanyika nchini China katika jiji la Sanya. Zaidi ya hapo, Tanzania imekuwa ikiishia katika hatua za awali kwenye shindano la dunia.

Kwa bahati nzuri, Nancy aliwaumbua wote waliowahi kusingizia ubaguzi au historia ya nchi yetu, pale alipowabwaga warembo wenzake wa Afrika na kutwaa umalkia wa bara hili.

Warembo Waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania

1967- Theresa Shayo

1994- Aina Maeda

1995- Emily Adolf

1996 Shose Sinare

1997 Saida Kessy

1998 Basila Mwanukuzi

1999 Hoyce Temu

2000 Jacqueline Ntuyabaliwe

2001      Happiness Magese

2002      Angela Damas

2003      Sylvia Bahame

2004 Faraja Kotta

2005 Nancy Sumari

2006 Wema Sepetu

2007 Richa Adhia

2008 Nasreen Karim

2009 Miriam Gerald

2010 Genevieve Emmanuel

2011 Salha Israel

2012      Lisa Jensen

2013 Brigitte Alfred

2014 Happiness Watimanywa

2015 Lilian Kamazima

 

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Boni Mwaitege amkalisha Mgogo

NA VALERY KIYUNGU KUPITIA shindano la Nani Zaidi linaloendeshwa na redio Passion Fm ya...

Mzuka warudi tena kwa s2kizzy

NA CHRISTOPHER MSEKENA SIKU chache baada ya kuvamiwa na kufanyiwa uharibifu wa studio zake za Pluto Republic, prodyuza nyota...

The Yeamen waipiga ‘Shoti’

NA JEREMIA ERNEST MSANII kutoka kundi la The Yeamen, Suma Toto, amewaomba mashabiki wa Bongo Fleva kuendelea kulipa sapoti...

JB Maeba atimiza ndoto zake na Cannibal

NA CHRISTOPHER MSEKENA MSANII wa Afro Pop na Bongo Fleva anayeishi Kenya, James Tesha a.k.a JB Maeba, amesema anafurahi...

‘Certified Lover Boy’ ya Drake yaiva

TORONTO, CANADA RAPA nyota ulimwenguni, Aubrey Graham maarufu kama Drake, ametangaza habari njema ya ujio wa albamu yake ya...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -