LONDON, England
KOCHA Pep Guardiola amedai kuwa Manchester City walikuwa na uwezo mkubwa katika ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Arsenal, kwani wageni wao walikuwa na bahati kuongoza kipindi cha kwanza.
Theo Walcott alifunga bao ambalo liliiwezesha Arsenal kuongoza dakika tano tu za mwanzo, lakini kama ilivyokuwa siku tano zilizopita dhidi ya Everton, walishindwa kung’ang’ania pointi tatu bila ya mafanikio na kuziacha zikipukutika.
Guardiola alipata mabao kipindi cha pili kupitia kwa nyota wake, Leroy Sane na Raheem Sterling ambao wana kila sababu ya kushukuriwa kwa kuipatia timu yao pointi tatu muhimu ingawa bado wapo nyuma ya vinara Chelsea kwa pengo la pointi saba.
Kocha huyo wa Kihispania anaamini timu yake ilistahili kupata ushindi dhidi ya Washika Mtutu.
“Sikuwaambia chochote kipindi cha mapumziko. Niliwaambia wasifikirie kuhusu kufunga, bali waendelee kucheza. Arsenal walikuwa na bahati kipindi cha kwanza,” aliiambia BBC Sport.
“Ilikuwa ni mechi ya Ligi ya Uingereza na mechi nzuri kwa kila mmoja. Ilikuwa sawa na mechi yetu dhidi ya Chelsea – tulicheza vizuri tukapoteza, lakini leo tumeshinda,” aliongeza kocha huyo.
Alisema kuwa walipata matokeo hayo kutokana na kuwa vijana wake walijitoa kamili kwa ajili ya ushindi na hivyo anafurahi kuwa kocha wa Man City.