Wednesday, October 28, 2020

Hapa ndipo tunapokosea kuhusu Kiba, Diamond

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA WARREN GERSON (TUDARCO)

POPOTE unapoanzisha mjadala wa nani bora kati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, hutapata majibu zaidi ya kuibua ugomvi kwa sababu wawili hawa wameugawa ulimwengu wa soka katika makundi mawili.

Kila upande unaamini katika ubora wa mchezaji wake na hauoni zuri lolote kutoka upande wa pili, kitu ambacho baadhi ya wachambuzi wa soka wanaamini si haki na kushauri badala ya kuwalinganisha dunia inatakiwa kuwaheshimu na kushukuru kwa kuwaona wakiwa uwanjani.

Lakini aina hii ya upinzani wa Messi na Ronaldo upo pia kwenye muziki wetu wa Bongo Fleva, watu wameacha kufurahia uwepo wa Ali Kiba na Nassib Abdul ‘Diamond’ na badala yake wanatumia nguvu nyingi kuwalinganisha na kuhoji nani bora kati yao huku wakitengeneza makundi mawili yasiyo na afya kwenye muziki wetu.

Mapya yanazidi kuibuka kuhusu ushindani wa Kiba na Diamond, ambapo mashabiki wa wasanii hawa wawili wanavutana huku kila moja akisema huyu ni bora na anamfunika mwenzake.

Binafsi huwa najiuliza je, kuna ulazima wa kujua nani bora kati ya Kiba na Diamond? Kwanini tusiishi na kufurahia ubora wao bila kujali tofauti zao? Kila nikiangalia ushindani wa wawili hawa kwa jicho la tatu sioni umuhimu wa kutumia nguvu nyingi kuwashindanisha.

Eti, mtu anadiriki kumponda Diamond kwa kutumia kigezo cha ukongwe wa Kiba! Au mtu unamkuta yuko ‘bize kum-dis’ Ali kwa sababu ya tuzo za kimataifa za Platnumz! Haniingii akilini.

Hakuna anayebisha kuwa Kiba ni mmoja kati ya magwiji wa Bongo Fleva na amekuwa na mchango mkubwa katika kuupaisha muziki huo tangu alipoanza kuvuma. Japo muziki wetu haukuwa na mafanikio hivyo, Ali alishiriki kwenye harakati za kuupa jina katikati ya miaka ya 2000, akianza na wimbo wake wa Cinderella.

Sitashangaa kusikia Diamond aliwahi kuziimba nyimbo za Ali Kiba kabla ya kujulikana kwake kimuziki sababu Kiba ndiye alianza kupata umaarufu kabla yake. Historia inasema Mondi alianza kupata jina mwaka 2009, wakati huo mwenzake tayari alikuwa na albamu mtaani.

Ubora wa Kiba ulionekana wazi baada ya kufanikiwa kufanya kazi na nguli wa muziki wa R&B ulimwenguni, Robert Kelly ‘R Kelly’, katika ‘project’ ya One8, kitu ambacho kilimtangaza kimataifa.

Lakini je, mafanikio haya si kigezo cha kukaa na kumsifia zaidi ya Kiba zaidi ya Diamond? Sidhani!

Kwa upande wa Diamond Platnumz akiwa chini ya Babu Tale na Mkubwa Fella, ni wazi kuwa uongozi wa wawili hao umemsaidia kufanya mambo makubwa sana kwenye muziki ndani na nje ya nchi.

Mbali na mafanikio yake binafsi, lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB) pia imekuwa ikitikisa tasnia ya muziki nchini kwa kuwasaini wasanii kama Harmonize na Raymond ambao kwa sasa ni kama alama ya lebo hiyo.

Mbali na mafanikio ya lebo yake, Diamond pia ni mmoja kati ya wasanii ambao wanatikisa Bara la Afrika na Ulaya kwa ujumla kutokana na kazi kuendelea kubamba kila kukicha.

Amekuwa akifanya mambo makubwa na ndiyo maana kila siku amekuwa akipiga shoo za kufa mtu ndani na nje ya nchi, huku akitwaa tuzo za kila aina tangu jina lake lilipoanza kufanya vizuri kimataifa na wimbo wa Number One remix alioimba na Davido.

Mafanikio ya Mondi kimataifa kwa kiasi kikubwa yamefungua milango ya wasanii wa Tanzania Bongo Fleva kufanya vizuri nje ya nchi, tumeshuhudia watu kama akina Vanessa Mdee nao wakifuata nyayo zake na kuipeperusha bendera ya Taifa letu.

Lakini pamoja na haya yote swali langu linabaki pale pale, je, anachofanya Diamond kimataifa kinafaa kumdhihaki Kiba? Siamini hili pia!

Binafsi natamani kuona Watanzania wakianza kujiuliza maswali sahihi kuhusu Kiba na Diamond, yaani badala ya kuhoji nani mkali kati yao, tunahitaji kuanza kujiuliza swali, je, mafanikio yao yana faida gani kwenye muziki wa Tanzania? Au kufanya kwao vizuri kunalinufaisha vipi Taifa?

Badala ya kuwaponda Diamond na Kiba, tunatakiwa kuanza kuwasifia kwa kuitangaza lugha yetu ya Taifa kimataifa kupitia muziki wao, kiasi cha kumshawishi mwanamuziki kama Yemi Yalade kuimba Kiswahili.

Kwa kifupi, mashabiki wanapaswa kutambua kwamba wasanii hawa wawili wote wana mchango mkubwa sana si katika tasnia hii ya muziki wa Bongo Fleva bali hata maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Kupitia muziki wao leo hii mtu kama Kiba amefikia hatua ya kuchangia kiasi cha Sh milioni 21 kwa GSM Foundation ikiwa ni kwa ajili ya kusaidia jitihada za taasisi hiyo ya kutoa huduma ya upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Vile vile inabidi tukumbuke mchango wa Diamond wa kutoa madawati kwa ajili ya wanafunzi shuleni na pia kujitolea kusomesha watoto wawili hadi elimu ya juu ngazi ya chuo kikuu.

Mashabiki wanatakiwa kupunguza kuwafananisha au kuwashindanisha wasanii hawa na inawapasa kutambua uwepo na mafanikio yao ikiwemo na michango yao ndani ya jamii yetu.

Ndiyo maana binafsi naungana na maneno ya Farid Kubanda ‘Fid Q’ kwenye wimbo wake wa Sumu, ambapo kuna mstari unasema ‘hawaamini kwenye kuunda Diamond au Kiba wawili, wanachoamini ni kumshusha mmoja ili mmoja awe dili’.

Ni kweli kabisa watu hawajui kuwa wanawahitaji wote Kiba na Mondi wawe juu, kazi yao ni kufikiria namna ya kumshusha mmoja kitu ambacho binafsi naamini ni makosa.

Kama mtu ukiwa mpenzi wa kweli wa muziki haiingii akilini kuona ukishindwa kukubali kazi za mmoja kati ya hawa wawili, nadhani wakati wa kuimba jina la Kiba na Diamond ni sasa, mambo ya kuendekeza ‘team’ zisizo na faida yamepitwa na wakati.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -