Friday, October 30, 2020

Hiki ndicho kinachomponza Diamond Platnumz

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA MICHAEL MAURUS,

DAKIKA kama si saa chache baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya wa Tanzania, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ kutwaa Tuzo ya Afrimma 2016, kupitia kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, wadau wa muziki na wengineo hapa nchini, haraka mno walianza kutoa maoni yao kupitia njia mbalimbali, zaidi ikiwa ni mitandao ya kijamii.

Hafla ya tukio hilo la kukabidhi tuzo, ilifanyika huko Dallas, jijini Texas, Marekani ambapo pia msanii mwingine wa Tanzania, Rajabu Ibrahim ‘Harmonize’, alitwaa Tuzo ya Msanii Bora Chipukizi, huku Mtanzania DJ D Ommy akiibuka kama DJ Bora wa Afrika.

Ukiachilia mbali Harmonize na DJ D Ommy, Diamond si mgeni kwenye tuzo hizo kwani alishatwaa miaka iliyopita kama ambavyo amekuwa akifanya katika tuzo nyinginezo nchini kama zile za KTMA, hasa zilizotolewa nje ya Tanzania.

Miongoni mwa tuzo ambazo Diamond ametwaa, zipo zile za Channel O, MTV-Base Africa maarufu kama MAMA, MTV EMA, BET na nyinginezo kutoka nchi mbalimbali.

Pamoja na kutwaa tuzo hizo, bado Diamond amekuwa hapewi heshima inayomstahili kutoka kwa baadhi ya Watanzania wenzake.

Japo ni ukweli kuwa si Watanzania wote wanaomshabikia Diamond, lakini inapotokea msanii huyo amefanya kitu kikubwa ambacho mwisho wa siku, kinabaki kuwa fahari ya Tanzania, si sahihi kuona kuna wengine wanamponda na kubeza mafanikio yake.

Binafsi juzi nilishuhudia katika moja ya mitandao ya kijamii baadhi ya vijana wa Tanzania ambao wamekuwa wakihaha kupambana na maisha angalau waweze kujiepusha na adha za vyumba vya kupanga, wakiponda mafanikio ya Diamond kupitia tuzo za Afrimma.

Tena mbaya zaidi, baadhi ya hao wanaomponda ni wale ambao wamekuwa wakiwahimiza vijana wenzao kujituma katika maeneo ya kazi kwa kutumia nguvu na akili zao zote waweze kujikwamua kimaisha.

Tena wakati mwingine, unaweza kukuta wanaombeza Diamond Platnumz wakiwa ni vijana wenye maisha ya kawaida kabisa ambao wakati mwingine, mlo mmoja tu wa siku huwa ni shida kwao.

Ukitafakari kwa makini, utabaini kuwa wanaomponda Diamond Platnumz ni wale ambao wanasahau kuwa mafanikio yake yametokana na kujituma kwake katika kazi yake.

Hao ni wale ambao wanachokumbuka wao ni wapi ametokea msanii huyo, hasa wanapokumbuka picha zake za utotoni akionekana kutoka katika familia duni, huku wakisahau kuwa hata wanasoka wa Kibrazil kama Ronaldo di Lima, Rivaldo, Neymar na wengineo au Mnigeria, Nwako Kanu na wengineo wengi, walitokea katika maisha duni kuliko hata ilivyokuwa kwa Dimaond na baadaye kuwa watu maarufu duniani wakimiliki fedha na mali za thamani kubwa.

Wakati mwingine pia unaweza kuwaza kuwa huenda wanaombeza Diamond kutokana na mafanikio yake wanafanya hivyo kwasababu tu msanii huyo ametokea katika mazingira ya kawaida kabisa ya Tandale na si Masaki, Mbezi Beach au Oysterbay.

Unaweza kujiuliza iwapo mafanikio anayoyapata Diamond Platnumz yangekuwa ni kwa msanii Ambwene Yesaya ‘AY’ aliyekulia Masaki, naye angekuwa akibezwa kiasi hicho?

Ni wazi jibu ni hapana. Sasa kwanini iwe hivyo kwa Diamond? Au ni kwasababu ‘Kwao ni Mbagala?’ Tafakari.

Mwisho wa siku, Watanzania ni vema wakafahamu kuwa mafanikio ya Diamond kama ilivyo kwa wengineo hapa nchini na kwingineko, hutokana na uwezo, jitihada, umakini, malengo pamoja na mapenzi dhidi ya shughuli husika.

Kama wewe ni mwandishi wa habari, ukiipenda kazi yako na kuifanya kwa kutumia akili na nguvu zako zote, lazima utafanikiwa.

Vile vile, kama wewe ni mwanamuziki, ukiifanya kazi yako kwa ufanisi na kuweka pembeni ubishoo, lazima utafanikiwa na kubeba tuzo lukuki kama ilivyo kwa Diamond.

Japo wapo baadhi ya Watanzania wanaombeza Diamond, lakini kuna wengine maarufu nje ya Tanzania wanaomkubali, kiasi cha kufikia hatua ya kumgombania kufanya naye kazi.

Hivi karibuni nilisoma katika moja ya mitandao kuwa msanii wa filamu wa Nollywood, Chinedu, maarufu kama Ukwa, amemmwagia sifa Diamond Platnumz kutokana na wimbo wake wa Salome alioutoa siku chache zilizopita akisema ameupenda mno.

Alisema japokuwa haelewi kinachoimbwa katika wimbo huo (lugha ya Kiswahili), lakini ni kazi nzuri kwa kila kitu.

Ikumbukwe kuwa Diamond Platnumz, amekuwa akitwaa tuzo hizo baada ya kuwapiga mweleka wasanii wengine wakali Afrika kama ilivyokuwa mwishoni mwa wiki huko Dallas.

Miongoni mwa wasanii waliowahi kuonja joto ya jiwe kutoka kwa Diamond kwenye tuzo mbalimabli ni T Pain na 2 Face wa Nigeria, Uhuru na Mafikizolo wa Afrika Kusini, Dr Sid wa Nigeria, Mkenya Amani, J Martins, Rebees na Wizkid.

Wengine ni Bebe Cool wa Uganda, Wyre wa Kenya, Navio wa Uganda na Jackie Gosee wa Ethiopia na wengineo.

Diamond Platnumz ametokea wapi?

Msanii huyo alizaliwa Oktoba 2, mwaka 1989 katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam, mnamo saa kumi na moja na kupewa jina la Nasibu Abdul, japo kwa sasa hupenda kuandika jina lake la kwanza Naseeb.

Kwa bahati mbaya, mkali huyo hakupata nafasi ya kufurahia maisha ya wazazi wake wote wawili baada ya wazazi wake kutengana akiwa na umri mdogo hivyo kulelewa na mama yake pekee.

Hapo ndipo mama yake alipoamua kuhamia kwa bibi wa msanii huyo maeneo ya Tandale yalikohamia makazi yao.

Katika moja ya machapisho ya historia ya msanii huyo, inaonyesha kuwa maisha yake ya utotoni yalikuwa ni ya kusikitisha kama alivyoimba katika wimbo wake wa Binadamu Wabaya.
Mwaka 1995 alianza kupata elimu ya awali katika Shule ya Chakula Bora, Tandale Uzuri, jijini Dar es Salaam na baadaye kujiunga na Shule ya Msingi Tandale Magharibi mwaka 1996.

Kama ilivyo kwa watoto wengi, kipaji cha Diamond katika muziki kilianza kujionyesha mwaka 2000 akiwa darasa la tano ambapo alianza kuonyesha dhahiri kuipenda fani hiyo kutokana na kuimba mashairi ya nyimbo za wanamuziki na bendi mbalimbali, ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu ya machapisho hayo ya historia ya mkali huyo, mama yake alikuwa akimnunulia kanda za wanamuziki mbalimbali waliokuwa wakitamba enzi hizo ili mwanaye aweze kukata kiu yake ya kuimba.

Imeelezwa kuwa wakati mwingine mama Diamond alikuwa akimwandikia mwanaye mashairi ya baadhi ya nyimbo za wanamuziki waliokuwa wakitamba, ikiwamo kumpeleka katika matamsha mbalimbali.

Tangu wakati huo, maisha ya Diamond yalimtegemea mama yake ambaye alilazimika kujinyima ili mwanaye aweze kushi, lakini pia kukata kiu yake aliyokuwa nayo katika kipaji cha muziki.

Lakini wakati Diamond akijiandaa kujiunga na elimu ya sekondari baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2002, mama yake alimtaka kuachana kabisa na muziki na kujikita kwenye elimu.

Kuna msemo wa kiswahili usemao kuwa kama ipo ipo tu; ndivyo ilivyokuwa kwa Diamond kwani akiwa sekondari, aliendelea kufanya muziki kwa siri bila mama yake kufahamu hadi mwaka 2004 alipoanza kuandika mashairi yake mwenyewe na kuyafanyia kazi.

Mwaka 2007, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kumaliza kidato cha nne, Diamond alielekeza nguvu zake zote katika muziki ambazo mwisho wa siku, zimemfikisha alipo leo hii, akiwa ni mmoja wa wasanii wakubwa wa muziki Afrika.

Hata hivyo, kuelekea mafanikio anayoyapata sasa ambayo wapo wanaomponda, Diamond amepitia katika vipindi vigumu mno, ikiwamo kusaka fedha kwa jasho hasa, ikiwamo kufikia hatua ya kuuza mitumba, kufanya kazi katika vituo vya mafuta, kupigisha simu, kupiga picha na hata kufanya kazi za viwandani.

Pia, Diamond alifikia hatua ya kujiingiza katika makundi ya kucheza kamari huko mitaani ili aweze kupata fedha za kumwezesha kurekodi nyimbo zake alizotunga na kuimba yeye mwenyewe.

Wimbo wake wa kwanza kabisa kuurekodi ulikuwa ni ule wa Toka Mwanzo. Lakini wanaomponda kwa sasa msanii huyo, wanafahamu alipata wapi fedha za kuingia studio kwa mara ya kwanza?  Usikose nakala yako ya BINGWA Jumanne ijayo kupata simulizi zaidi juu ya safari ya Diamond Platnumz kuelekea katika mafanikio aliyonayo sasa ambayo leo hii, wapo wanaokesha kwenye mitandao ya kijamii kumponda.

Kama una maoni juu ya makala haya, changia kwa sms kupitia namba 0622 556022 au anuani pepe; michietz@yahoo.com.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -