Wednesday, October 28, 2020

Huyu ndiye Mustafi ‘orijino’

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

LONDON, England

AKIWA ndio kwanza ana umri wa miaka 24, Shkodran Mustafi, amefanikiwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Arsenal na hajaonja machungu ya kupoteza mchezo tangu alipotua klabuni hapo akitokea Valencia.

Nyota huyo alikulia sehemu inayoitwa Bad Hersfeld ambao ni mji mdogo nchini Ujerumani. Kutoka alipozaliwa mpaka Frankfurt ni mwendo wa saa moja na nusu kwa gari. “Nilikulia pale nikiwa na kaka yangu, watoto wa dada zangu na familia yote, ilikuwa poa sana,” alisema Mustafi.

Ule msemo wa Kiswahili wa mtoto wa nyoka ni nyoka uko wazi kwenye historia ya soka ya Mustafi ambaye anadai kuwa hata baba yake pia aliwahi kucheza kandanda.

Hata hivyo, tofauti na wazazi wengine ambao hupenda kuwalazimisha watoto wao kufanya kazi wanazofanya wao, baba yake Mustafi hakumlazimisha mtoto wake huyo kucheza soka.

“Sikuwa nikilazimishwa (kucheza soka). Baba yangu alikuwa mchezaji na aliupenda sana mchezo huo lakini sikuwa nikilazimishwa kuwa mwanasoka. Lilikuwa jambo zuri.

“Nilipotaka viatu vipya vya mpira, alinunua kila alipokuwa na uwezo wa kifedha kwa sababu kuna kipindi hakuwa na fedha. Alijaribu kunichukua kila sehemu aliyokwenda, kwenye mechi na hata mazoezini, lakini hakuwa akinilazimisha kucheza soka. Hakuwa akininunulia viatu na kuniambia ‘ufunge mabao 10, la sivyo sitokununulia tena’.

“Nimekuwa nikiwaona wazazi wengi wakiwalazimisha watoto wao (kufanya kazi fulani) na nafikiri hilo huua vipaji vya watoto hao,” alisema Mustafi.

Mustafi ambaye alizaliwa Ujerumani huku wazazi wake wakiwa ni raia wa Albania, ana uwezo wa kuzungumza lugha tano na mara kadhaa amekuwa akitumia muda wake wa mapumziko kwenda Albania.

Licha ya kuombwa kuichezea timu ya Taifa ya Albania ambayo hata yeye amewahi kukiri kujivunia nchi hiyo, Mustafi aliamua kuichezea Ujerumani na alikuwa sehemu ya kikosi hicho kilichotwaa taji la fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.

“Ni suala la kufanya uamuzi na kuamua kusimamia ulichoamua,” alisema Mustafi akizungumzia uamuzi wake wa kuichezea Ujerumani badala ya Albania.

“Nilifanya uamuzi wa kuichezea Ujerumani kwa sababu nchi hii ilinifanyia kitu cha kipekee na ilinisaidia katika soka langu la utotoni.

“Nilipoitwa na Albania, nilizungumza na kocha lakini nilishaamua. Nilijiona wa pekee kwa kipindi hicho kwa sababu wazazi wangu walikulia pale na mimi pia ni wa pale na mara kadhaa huwa nakwenda kuiona familia yangu, lakini kwa upande wangu hakukuwa na uwezekano wa kubadili mawazo.”

Akiwa kwenye kikosi cha vijana, Mustafi aliichezea Ujerumani zaidi ya michezo 60 na tayari hivi sasa ana uzoefu mkubwa licha ya kuwa na umri wa chini ya miaka 25.

Mustafi aliamua kuikacha ‘academy’ ya Hamburg ya Ujerumani na kujiunga na ile ya Everton na hiyo ilikuwa mwaka 2009, lakini alishindwa kupenya na kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo ya jijini Merseyside, England.

“Kwangu, (kucheza timu ya taifa) nikiwa na umri wa miaka 17 kulinisaidia sana, hivyo nilipokwenda Everton nilitegemea kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza na kucheza soka la juu. Lakini nilijikuta nikicheza kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba na haikuwa kwa ubora wa juu.

Alipochomoka Everton, nyota huyo alikimbilia Italia na kujiunga na Sampdoria na baadaye alitua Hispania alikosajiliwa na Valencia kabla ya ujio wake wa pili England na safari hii akijiunga na Gunners. Mbali na uzoefu, kuhama huko kulimwezesha Mustafi kujifunza lugha mbalimbali.

Katika mchezo wa hivi karibuni wa Ligi Kuu England dhidi ya Middlesbrough, akicheza sehemu kubwa ya mchezo huo kwenye eneo la kiungo, Mustafi alionekana kuwa hatari zaidi kwa wapinzani wao hao na alikuwa mmoja kati ya wachezaji wawili pekee waliogusa mpira mara nyingi.

Tofauti na John Stones wa Manchester City ambaye amekuwa akilaumiwa kwa kukaa na mipira na hata kupoteza katika eneo la hatari, Mustafi ameonekana kulimudu vyema jukumu hilo.

“Unapoichezea Arsenal, unatakiwa ucheze na ndivyo soka la kisasa linavyotaka. Hata beki wa kulia, beki wa kushoto na mlinda mlango, wote wanatakiwa kucheza na kupandisha mashambulizi. Timu kubwa zinataka makipa ambao si wazuri tu langoni lakini pia waweze kuuchezea mpira.

“Kama unataka timu yako icheze lazima uwe na wachezaji wa nyuma wanaoweza kufanya hivyo. Inaipa timu ubora mkubwa kwa sababu unawaambia wachezaji kuwa wanatakiwa kuchukua mpira kutoka kwa kipa na kusonga mbele wenyewe,” alisema Mustafi.

Akiwa na uzoefu mkubwa kutokana na kucheza Serie A na La Liga, EPL ni ligi yake ya tatu kubwa.

Mara kadhaa amekuwa akikiri kuwa amekuwa shabiki mkubwa wa soka la England ingawa amekiri wazi kuwa ana kibarua kizito kuikabili mikiki mikiki ya ligi.

Hata hivyo, anaamini kuwa timu za Ligi Kuu England zinatakiwa kukaza buti hasa katika masuala ya kiufundi ili kushindana na wapinzani wao kutoka ligi nyingine.

“Hata kama unawafunga mabao mengi, timu za England hazina kawaida ya kukata tamaa, watapata moja na kuanza kuamka upya. Hicho ndicho ninachokipenda kwenye soka la England, timu zinapambana hadi dakika ya mwisho.

“Kwangu ufundi ni pale timu nzima inapokuwa na wazo moja. Kama ukiiangalia Atletico Madrid kwa miaka michache iliyopita, hakuna aliyejali kuhusu timu hiyo kwani haikuwa na wachezaji wenye majina makubwa lakini hakuna asiyeijua shughuli yake uwanjani,” alisema Mustafi.

“Unaweza kuwa na mastaa wengi kikosini lakini kama watashindwa kucheza kitimu basi ni ngumu kwa timu kupata ushindi.

“Mara nyingi kuusoma mchezo na kuwa mjanja kiufundi kunarahisisha kazi hasa kwenye safu ya ulinzi na kama unapata mpira ni rahisi kuipandisha timu kuelekea kwenye lango la timu pinzani.”

Mustafi alielezea furaha yake ya kujiunga na Wajaremani wenzake Per Mertesacker na Mesut Ozil pale Emirates na alikiri kuwa hakudhani kama ingekuwa rahisi kulizoea soka la England.

Akilizungumzia hilo, Mustafi alisema: “Kutulia kwenye timu ilikuwa rahisi kwa sababu nilikuwa nikiwajua Per, Mesut na baadhi ya wachezaji wengine wachache, lakini unapokuja kwenye mji tofauti utatulia pale utakapopata nyumba.

“Baada ya kupata nyumba, unapokuwa umetulia ndipo utakapoanza kugundua matatizo madogo madogo, mara utajua huna kijiko, kisu na baadaye utagundua kuwa umekamilisha kila kitu.

“Utakapotaka kunywa maji, ghafla utagundua kuwa huna glasi na hapo ndipo utakapoinunua. Kwa kweli Arsenal wanakusaidia lakini hawawezi kukuchagulia sehemu unayotaka kuishi. (Arsenal) watakuja pindi utakapowahitaji lakini mambo mengine yanakuhusu wewe mwenyewe.”

Uwanjani mambo yameonekana kumnyookea Mustafi na Arsenal kwa ujumla, kwani tayari timu hiyo imecheza michezo 16 bila kukumbana na machungu ya kufungwa.

Kwa kiasi kikubwa siri ya mafanikio hayo ni safu imara ya ulinzi inayoundwa na Mustafi na beki mwenzake raia wa Ufaransa, Laurent Koscielny.

“Nafikiri ni pongezi inayotakiwa kutolewa kwa timu nzima. Tunachofanya vizuri ni kuusoma mchezo na kutumia akili. Tumepokonya mipira mingi na kujipanga vyema katika ulinzi,” alisema.

“Ni jambo la kuvutia kutofungwa mpaka sasa lakini unapaswa kufikiria kuwa unapopoteza mchezo mmoja hayo yote yatasahaulika. Unachotakiwa kukifanya ni kuachana na yaliyopita na kuhakikisha unashinda mchezo unaofuata, la sivyo kila tulichokifanya kitakuwa kazi bure. Tunachotakiwa kukifanya ni kuendelea kufanya vizuri na kuimarika zaidi.”

Kwa upande mwingine, kwa wanaomjua Mustafi wanafahamu fika kuwa amekuwa muwazi kuzungumzia masuala ya dini yake. Kama ilivyo kwa Ozil, staa huyo ni muumini mzuri wa dini ya Kiislamu na mara kadhaa amekuwa akiingia msikitini kufanya ibada.

“Mara nyingi binadamu huwa tunasahau kila kitu. Ukiwa kama binadamu, kwa sasa utataka kula, utataka kinywaji na utakapopata kahawa utataka zaidi ya hapo. Muda mwingine dini hukufundisha kuwa unatakiwa kushukuru kwa kile ulichonacho, unatakiwa kushukuru kwa kuwa mwanasoka.

“Hata kama huchezi vizuri, shukuru kwa kuwa kuna aliyekupa nafasi ya kufanya hivyo, furahia hilo. Kwangu dini yangu ndio kila kitu, kwa sababu inafundisha kushukuru kwa kile ulichojaaliwa na hapo ndipo utakapopata zaidi. Kuwasaidia watu, unatakiwa kuwasaidia wachezaji wenzako ndani na nje ya uwanja.

“Na kuwaheshimu watu wengine. Hasa katika biashara hii (soka), unatakiwa kuendelea kujitunza mwenyewe na kujaribu kwasaidia wengine, hata kama kuna muda unakuwa na mambo mengi ya kufanya.

“Muda mwingine unaweza kuwa sehemu ambayo hakuna anayekujua kama wewe ni Mustafi. Unaangalia mpira kwa dakika 90 na hujui Mustafi ni yupi. Dini inanifanya niwe mimi na si kuwa Mustafi ambaye anajulikana.

“Nilikuwa kwenye familia ambayo dini ilikuwa ni kitu mihumu kuliko vyote. Dini ni kama soka, kama huamini kile unachokifanya, basi umekwisha kwa sababu hakuna cha maana kitakachotokea.”

Akisimulia alipokuwa Everton, Mustafi anasema wachezaji wengi wa timu hiyo walimshangaa kwa kitendo chake cha kuipotezea pombe na kwa mujibu wake jambo hilo limemsaidia kwa kiwango kikubwa.

“Nilipokuwa na umri wa miaka 17, nikiwa na Everton, niliwahi kutoka na wachezaji wenzangu ambao wengi wao walinijua kuwa mimi ni Mjerumani.

“Mara kadhaa walikuwa wakiniuliza: ‘Wewe ni Mjerumani, imewezekana vipi hunywi pombe?’ Niliwajibu, ‘hapana, mimi ni Muislamu na sinywi pombe’.

“Waliniuliza pia, ‘kwanini wewe ni Muislamu?’ na niliwajibu, ‘ndiyo, wazazi wangu ni waislamu na nilikua kwenye familia ya Kiislamu’.

“Nilipofika nyumbani niligundua kuwa maswali yale yalikuwa mazuri kwa sababu sikuwahi kujiuliza. Ni kitu ambacho wazazi wako wanakufundisha lakini huwezi kujua kama ni kizuri au kibaya. Kwanini sinywi pombe, kwanini sili nguruwe na kwanini natakiwa kuswali mara tano kwa siku. Nilianza kusoma Qur’an na ndipo nilipoanza kuwauliza (wazazi) maswali mengi tu.

Anapokuwa hachezi mazoezi au mechi, Mustafi si mzururaji kama walivyo wachezaji wengine na badala yake amekuwa akipendelea kukaa na familia yake au marafiki zake.

“Kucheza kila baada ya siku tatu kunakufanya ukose muda mwingi nje ya uwanja. Huwa nachoka sana, hivyo nafurahia kukaa na familia na kuzungumza na washikaji,” alisema.

“Muda mwingine baada ya mazoezi unapiga picha na kufanya mahojiano na waandishi wa habari. Huweza kuchukua muda mwingi na ukija kushituka utakuta muda umekwisha. Si kukaa tu nyumbani na kukosa cha kufanya, hakuna muda ambao utakosa cha kufanya.”

 

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -