NA MWANDISHI WETU
MOJA kati ya vitu vilivyorahisisha utengenezaji wa filamu ya mapigano ya The Foundation (Msingi), ni ukuaji wa teknolojia ya utengenezaji wa filamu nchini, anasema mwandaaji wa filamu hiyo, Jimmy Mponda, ‘J- Plus’.
J-Plus aliliambia PAPASO LA BURUDANI kuwa, zamani ilikuwa ngumu sana kutengeneza filamu za mapigano nchini kutokana na kukosekana kwa teknolojia nzuri ya kufanikisha zoezi hilo, kitu ambacho ni tofauti na sasa.
“Nakumbuka enzi zile tunatengeneza Misukusuko, kazi ilikuwa ngumu sana,” alisema J-Plus na kuongeza: “Lakini safari hii kutokana na ukuaji wa teknolojia, baadhi ya mambo yamerahisishwa, hivyo ni rahisi kupata ubora unaotakiwa kwenye filamu za ‘action’ (Mapigano).”
Filamu ya kibabe ya The Foundation inatarajiwa kuingia sokoni Jumatatu hii na ndani ya muvi hiyo kwa mara nyingine tena J-Plus na Sebastian Mwanangulo ‘Seba’, wanatarajia kukutana tena baada ya kufanya makubwa sana katika Misukosuko miaka ya nyuma.