LONDON, England
Harry Kane amesaini mkataba mpya kwenye klabu yake ya Tottenham utakaomfunga hadi mwaka 2022.
Kane ambaye alikuwa kinara wa mabao msimu uliopita wa Ligi Kuu England akitingisha nyavu mara 25, amekuwa kwenye mazungumzo na Spurs tangu majira ya kiangazi na kuamua kuongeza miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa utakaomfanya abakie White Hart Lane hadi mwaka 2022.
“Ni jambo la kufurahisha na kila mmoja anajua jinsi ninavyoipenda hii klabu,” alisema Kane akizungumza na mtandao wa klabu hiyo ya Tottenham.
“Kusaini mkataba mpya ni kitu kizuri. Tuna kikosi kizuri chenye chipukizi wengi na klabu ina mwelekeo mzuri.”
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ni mchezaji mwingine kwenye klabu hiyo ya White Hart Lane kuongeza mkataba, baada ya nyota kama Christian Erisken, Dele Alli, Kyle Walker, Danny Rose, Eric Dier na Harry Winks kukubali kuendelea kukipiga katika klabu hiyo ya London.