Na kidawa Hassan (out)
MKALI wa muziki wa Bongo Fleva nchini, Ali Kiba, amesema moja ya mafanikio ambayo anajivunia kwa mwaka huu ni kushiriki tena onyesho la Coke Studio.
Kiba ambaye amefanya kolabo na mwimbaji wa Nigeria, Patoranking, amesema kushiriki msimu huu wa tano wa Coke Studio kutamfanya aongeze mashabiki na kujiongezea umaarufu.
“Kushiriki katika onyesho hili linaloandaliwa na kampuni kubwa ya vinywaji ya Coca Cola pamoja na kushirikiana na Patoranking kunanifanya niongeze mashabiki na umaarufu wangu kuongezeka,” alisema Kiba.
Alisema onyesho la Coke Studio linadhihirisha kuwa Bongo Fleva inazidi kukua na kupata umaarufu sehemu mbalimbali barani Afrika kutokana na jinsi linavyofuatiliwa na idadi kubwa ya mashabiki hasa vijana.
Aliwataka wanamuziki wachanga wanaochipukia kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanapata mafanikio na kuongeza kuwa mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi na makampuni makubwa ya biashara, mojawapo ikiwa ni kushiriki kwenye maonyesho makubwa kama haya.
Pia Kiba aliwapongeza wasanii wenzake kutoka Tanzania ambao wamepata nafasi ya kushiriki onyesho hilo la Coke Studio linaloonyeshwa kila Jumamosi kwenye Runinga ya Clouds, ambapo wasanii hao ni Rayvanny, Izzo Bizness na Nandy.