NA MWANDISHI WETU
WASANII mahiri hapa nchini, Ali Kiba, Ben Pol, Jux, Nandy na Maua, wanatarajiwa kutoa shoo kwa kutumia vyombo (live) katika tamasha la Tigo Fiesta ambalo wikiendi hii litarindima kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugrenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, lengo la kufanya hivyo ni kutoa burudani halisi kwa wapenzi wa muziki na burudani kwa ujumla watakaohudhuria tamasha hilo kubwa kabisa na la aina yake hapa nchini.
Aliwataja wasanii wengine watakaopanda jukwaani na kufanya muziki wa ‘live’ Mwanza kuwa ni kundi la Weusi, mkali wa Hip Hop nchini Fid Q na ‘kichwa’ cha Bongo Fleva Rayvanny, huku watakaotumia CD wakiwa ni Aslay, Young Killer, Rosa Ree, Lulu Diva, Darasa, Rostam, Bill Nas, Future JNL, Bright, Eduboy na wengineo.
Alisema tamasha hilo lenye kaulimbiu ya ‘Tumekusomaa’ ambalo ni la 16, linatarajiwa kutua katika miji 15 ambapo hadi sasa, tayari limeshatimua vumbi miji mitatu ambayo ni Arusha, Musoma na Kahama na kwamba baada ya Mwanza, litahamia Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.
“Kupitia Tigo Fiesta 2017- Tumekusoma, Tigo imejikita kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa nchini. Kama tunavyojua, sanaa imekuwa mojawapo ya nafasi kubwa za ajira kwa vijana wetu na baaadhi ya wasanii wetu pia wamepata nafasi ya kuperusha bendera ya nchi katika nchi za kigeni, kwa hiyo kusaidia kuitangaza nchi yetu,” alisema Mpinga.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Fiesta, Sebastian Maganga, alisema kuwa wakazi wa Mwanza watarajie shoo kabambe na ya aina yake kutoka kwa wasanii wao wakali wa hapa nchini.
“Tutawaletea wasanii wenye hadhi kulingana na mapendekezo ya mashabiki husika wa mkoa huo, tena wale waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi,” anasema Maganga.