NA WINFRIDA MTOI
WINGA wa Simba, Shiza Ramadhan ‘Kichuya’, amesema wanatarajia kuanza upya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuhakikisha wanapata matokeo bora zaidi ili waweze kutimiza malengo yao ya kuchukua ubingwa.
Simba wataanza na Ndanda katika mchezo wa mzunguko huo, utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara, baada ya mzunguko wa kwanza kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA juzi, Kichuya alisema anachohitaji ni kutaka kuanza ushindi mnono zaidi ili aweze kuendelea kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo.
Kichuya alisema anajua wazi kuwa anaingia kwenye mpambano mpya wenye changamoto kuliko mechi zilizopita, kutokana na klabu nyingi kufanya usajili wa kuimarisha vikosi vyao.
“Tunakoelekea ni kama tunaanza upya ligi, kwa sababu kila timu imejipanga, ukizingatia wachezaji wamepata mapumziko ya kutosha na watarudi na nguvu nyingine, mechi zinakuwa ngumu tofauti na mzunguko wa kwanza,” alisema Kichuya.
Kichuya alisema kwa sasa anazingatia mazoezi anayopewa na makocha wake na yaliyopita katika duru ya kwanza hayapo kichwani mwake, zaidi ya kufikiria jinsi ya kuanza mzunguko wa pili.
Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 35, wakifuatiwa na watani wao wa jadi, Yanga wenye pointi 33, ambao kesho watacheza na JKT Ruvu Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.