MANCHESTER, England
JUZI ilikuwa siku mbaya kwa mashabiki wa klabu ya Liverpool kwa kukishuhudia kikosi chao kikichapwa mabao 5-0 na Manchester City.
Mbaya zaidi kwa Liver ni kumpoteza staa wao, Sadio Mane, aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 37 ya mtanange huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Etihad.
Fowadi huyo wa kimataifa wa Senegal alikumbana na adhabu hiyo kutoka kwa mwamuzi, Jon Moss, baada ya kumchezea rafu mlinda mlango wa Man City, Ederson.
Mpaka Mane anatolewa uwanjani, Man City walikuwa mbele kwa bao 1-0 kupitia kwa mshambuliaji wao raia wa Argentina, Sergio Aguero.
Kutoka kwa Mane lilikuwa pigo kubwa kwa Liver kwani walishindwa kuzuia mabao mengine mawili kutoka kwa Gabriel Jesus na jingine kutoka kwa Leroy Sane.
Hata hivyo, hakikuwa kupoteza pointi tatu tu, bali matokeo hayo yalikuwa na rekodi nyingi kwa Man City dhidi ya Liver.
Kwanza, kilikuwa ni kipigo cha kwanza kizito kwa kocha Jurgen Klopp tangu alipotua England Oktoba 2015. Kichapo cha juzi kilizidi kile cha mwaka huo, ambapo Liver ya mkufunzi huyo ilichapwa mabao 3-0 ikiwa ugenini dhidi ya Watford.
Pili, kabla ya kuvuliwa nguo na Man City, Klopp hakuwahi kufungwa mabao matano kwa kipindi cha miaka 11. Kwa mara ya mwisho, alikutana na balaa hilo mwaka 2006 akiwa na Mainz ya Bundesliga, ambapo alichezea kichapo cha mabao 6-1 kutoka kwa Werder Bremen.
Man City pia walimwaribia Klopp rekodi yake ya kutamba ugenini kwani hakuwa amepoteza katika mechi tisa zilizopita dhidi ya timu vigogo. Katika idadi hiyo ya michezo, Mjerumani huyo alikuwa ameshinda mara tano na kutoa sare nne.
Mbali na hiyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya Liver, ilichapwa mabao 5-0. Haijawahi kutokea katika mechi za Ligi Kuu England. Kichapo chao kikubwa kilikuwa katika msimu wa 2014-15 walipofungwa mabao 6-1 na Stoke City.
Takwimu zinaonyesha pia tangu miaka ya 1990, juzi ilikuwa mara ya kwanza kwa Liver kuchapwa mabao mengi dhidi ya Man City. Kwa mara ya kwanza, Man City waliichapa Liver mabao 5-1 mwaka 1937.
Juzi ilikuwa siku mbaya zaidi kwa Liver kwani wachezaji wa kikosi hicho hawakupata nafasi ya kupiga shuti hadi ilipofika dakika ya 31 na dakika sita baadaye ndipo Mane alipolimwa kadi nyekundu.
Ilikuwa siku ya majonzi pia kwa staa mpya wa Arsenal, Alex Oxlade-Chamberlain, ambaye tangu kuanza kwa msimu huu ameshachapwa mabao 9-0.
Katika mchezo wa kwanza akiwa na Arsenal, timu yake hiyo ilifungwa mabao 4-0 na Liver, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Anfield na juzi akiwa kwenye kikosi hicho cha Klopp akakumbana na mabao 5-0 kutoka kwa Man City.
Man City na Liver zitakuwa dimbani keshokutwa kwenye michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wakati vijana hao wa Etihad wakipepetana na Feyenoord ya Uholanzi, wakali wa Anfiled watakipiga na Sevilla ya La Liga.