London, England
Leicester City wameendelea na kasi yao katika mchezo wao wa juzi Jumanne na sasa wana asilimia 100 ya kuweza kutinga hatua ya mtoano katika msimu wao wa kwanza kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Real Madrid, Borussia Dortmund, Juventus na Sevilla wakiungana na mabingwa hao wa Ligi Kuu England kwenye uwezekano wa kutinga hatua hiyo ya 16 bora.
Kundi E
Bayer Leverkusen 0-0 Tottenham Hotspur
Leverkusen walitawala mchezo huo lakini walishindwa kutingisha nyavu za mlinda mlango wa Tottenham, Hugo Lloris wakati wenyeji hao wakiendelea na rekodi yao ya kutoka sare ya tatu kwenye hatua za makundi. Vincent Janssen aligongesha mwamba kwenye lango la Spurs, ambao walinyakua pointi moja dhidi ya Leverkusen wanaoshika nafasi ya tatu.
CSKA Moskva 1-1 Monaco
Mlinda mlango wa CSKA Moskva, Igor Akinfeev, alikaribia kumaliza mechi yake ya kwanza bila ya kufungwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu Novemba 1 mwaka 2006, akicheza mechi 40 lakini dakika tatu kabla ya mchezo kumalizika Bernardo Silva aliharibu rekodi ya muongo mmoja iliyokaribiwa kuwekwa na mlinda mlango huyo baada ya kufunga bao la kusawazisha. Nyota anayekipiga CSKA Moskva kwa mkopo, Lacina Traore aliifunga klabu yake ya Monaco, ambao bado wanabakia kileleni huku CSKA wakiburuza mkia kwenye kundi hilo.
Kundi F
Real Madrid 5-1 Legia Warsawa
Legia walionekana kuanza vizuri msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mpaka sasa hawana pointi kabisa wakati Madrid wakijikusanyia pointi saba. Mabao matatu yalipatikana ndani ya dakika saba kutoka sare 0-0 mpaka 2-1, bao la Gareth Bale kisha Legia wakajifunga na kupata penalti iliyopigwa Miroslav Radovic. Marco Asensio alifanya matokeo kuwa 3-1 kabla ya mapumziko na Lucas Vazquez na mshambuliaji aliyeingia akitokea benchi Alvaro Morata waliongeza mabao mengine.
Sporting CP 1-2 Borussia Dortmund
Dortmund wamefunga kwa pointi saba na Madrid, wakiwapita Sporting kwa pointi nne baada ya bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang na lile la Julian Weigl lilitosha kuwapa ushindi pamoja na Bruno Cesar kuifungia Sporting kwa mpira wa adhabu. Ushindi mwingine wa Dortmund kwenye mechi ijayo itaipa timu nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano.
Kundi G
Leicester City 1-0 Kobenhavn
Bao la Riyad Mahrez kipindi cha kwanza lilitosha kuwafanya mabingwa hao wa Ligi Kuu England kuwa na msimu wa kwanza mzuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kushinda mechi yao ya tatu mfululizo kwenye hatua ya makundi, ambapo waliichapa 1-0 FCK inayoshika nafasi ya pili. Ushindi mwingine mjini Copenhagen utawafanya Leicester kutinga hatua ya 16.
Club Brugge 1-2 Porto
Penalti ya Andre Silva iliisaidia Porto kufungana kwa pointi na FCK walioko nafasi ya pili na kuifanya Brugge kubakia bila ya pointi. Klabu hiyo ya Ubelgiji, Brugge ilikuwa ikiongoza hadi Miguel Layun aliposwazisha dakika ya 22 kabla ya mchezo kumalizika, ambao bao lao la kuongoza lilifungwa na Jelle Vossen ikiwa ni bao la kwanza la Brugge kwenye hatua ya makundi.
Kundi H
Lyon 0-1 Juventus
Akitokea benchi Juan Cuadrado alifunga bao dakika 14 kabla mchezo huo kumalizika na wakiwa pungufu ya mtu mmoja, Juventus walifanikiwa kupata pointi dhidi ya timu inayoshika nafasi ya tatu Lyon. Mlinda mlango Gianluigi Buffon alicheza penalti ya Alexandre Lacazette kabla ya Mario Lemina kutolewa dakika ya 54, mkongwe huyo wa Juve, Buffon aliendelea kuwabania Lyon baada ya shuti la Nabil Fekir.
Dinamo Zagreb 0-1 Sevilla
Bao la Samir Nasri dakika ya 38 liliwafanya Sevilla kulingana pointi na Juve wakifikisha pointi saba na kuichapa Dinamo bao 1-0 kikiwa kipigo cha tatu bila ya kupata bao. Ushindi huo nyumbani kwa Dinamo, unaweza ukaibeba Sevilla hatua ya mtoano na kukwamisha ndoto yao ya kunyakua taji la Ligi ya Europa kwa mara ya nne mfululizo.