NA SAADA SALIM
STRAIKA wa Simba, Juma Luizio, amewaambia Yanga wafanye wanalojua lakini mwisho wa siku watakapokutana watawaachia pointi tatu na kuwarudisha kileleni.
Simba na Yanga zitashuka dimbani Februari 25 katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara, litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 48, ikitofautiana kwa pointi moja na wapinzani wake Yanga iliyo kileleni ikiwa na pointi 49.
Luizio ameliambia BINGWA kuwa hatua ya kuachwa pointi moja na mahasimu wao hao haina maana ndio wameondolewa katika kinyang’anyiro cha ubingwa msimu huu, badala yake anaamini vita bado kali baina yao.
“Mechi bado nyingi, ni mategemeo yangu baada ya ushindi dhidi ya Majimaji, kasi yetu itakuwa hiyo hiyo mpaka mwisho wa msimu, nataka kuwaambia Yanga kuwa waruke ruke lakini tutakapokutana wajiandae kuturudisha kileleni,” alisema.
Luizio alisema licha ya upinzani mkali wanaoutarajia katika mechi zao zijazo, bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kutwaa ubingwa msimu huu.