LONDON, England
LEO macho na masikio ya mashabiki wa Ligi Kuu England yataelekezwa kwenye Uwanja wa Anfield ambapo wenyeji Liverpool watakuwa wakiwakaribisha Chelsea.
Haitokuwa kazi nyepesi kwa Liver kubaki na pointi tatu kwani msimu huu Chelsea wameonekana kuja kivingine hasa baada ya ujio wa kocha Antonio Conte.
Lakini, mashabiki wa Liver watakuwa wakijivunia kurejea kwa ‘fundi’ wao Sadio Mane ambaye alikuwa Afrika kwenye michuano ya Afcon 2017.
Liver wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, baada ya kujikusanyia pointi 45.
Wapinzani wao Chelsea wako kileleni wakiwa na pointi 55 walizochuma katika michezo 22.
Katika mechi ambayo Chelsea imecheza na Liver pale Anfield, Chelsea wameshinda mara 13, huku wenyeji hao wakiibuka na ushindi katika michezo 48.
Lakini sasa, Chelsea hawajapoteza mechi tano zilizopita ambazo wamefika uwanjani hapo.
Idadi hiyo ilishuhudia wakishinda mara mbili na kutoa sare tatu.