Saturday, October 31, 2020

Mambo matano yanayomshitaki Pluijm Yanga

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA MICHAEL MAURUS

YANGA Jumamosi iliyopita ilishindwa kwa mara nyingine kufuta aibu ya kipigo cha kihistoria walichopewa na watani wao wa jadi, Simba cha mabao 6-0, pale walipojikuta wakilazimishwa sare ya bao 1-1, pamoja na kutangulia kupata bao la mapema kipindi cha kwanza.

Wakiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 26 na Amis Tambwe, Yanga ilipata nafasi ya kulipiza kisasi cha kipigo hicho kikubwa zaidi walichokipata mwaka 1977 kutoka kwa watani wao hao wa jadi, ambao walijikuta wakicheza wakiwa pungufu baada ya nahodha wao, Jonas Mkude, kuonyeshwa kadi nyekundu.

Mkude alitolewa uwanjani kwa kadi hiyo kwa kile kilichodaiwa kumpiga mwamuzi Martin Saanya, wakati akiwa na wachezaji wenzake waliokuwa wakimzonga refa huyo kwa kukubali bao la Tambwe kwa madai mfungaji alikuwa ameunawa mpira kabla ya kufunga.

Baada ya kutolewa kwa Mkude, mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba, walianzisha vurugu na kung’oa viti vya Uwanja wa Taifa, kabla ya kutulizwa na askari waliokuwapo uwanjani hapo.

Wakati hata vurugu hizo zikiwa hazijatulia, Saanya alipuliza kipyenga kuashiria kuendelea kwa mchezo huo, huku Yanga wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Tofauti na wengi walivyotegemea, Yanga walishindwa kutumia faida ya kucheza dhidi ya wapinzani wao waliokuwa pungufu, tena wakiwa wameondokewa na nahodha wao uwanjani, huku pia mashabiki wake wakiwa wametoka kwenye vurugu.

Badala ya kujipanga na kuongeza mashambulizi kuwachanganya zaidi wapinzani wao na hivyo kupiga mabao zaidi na ikiwezekana kutumia mwanya huo kulipiza kisasi cha kipigo cha mabao 6-0, wachezaji wa Yanga walianza kucheza kwa mbwembwe, wakijiona kama wapo mbele kwa mabao 7-0.

Wachezaji hao wa Yanga, walisahau kuwa wanacheza dhidi ya timu iliyosukwa upya, iliyosheheni vijana wenye vipaji vya hali ya juu na wapambanaji.

Pia, walisahau kuwa wanacheza na timu iliyojengeka mno kihamasa, kuanzia kwa wachezaji, viongozi hadi mashabiki wake.

Wachezaji wa Yanga walisahau kuwa pamoja na kuitambia Simba msimu uliopita katika michezo yote miwili, bado timu hiyo huwa inakuwa ‘imeshinda’ hata kabla ya mchezo inapocheza na Wanajangwani hao.

Matokeo yake, mashabiki wa Yanga walijikuta wakishindwa kuamini kilichotokea uwanjani baada ya winga hatari wa Simba, Shiza Kichuya, kuisawazishia timu yake bao dakika ya 42, alipochonga kona iliyotinga moja kwa moja nyavuni na kumwacha kipa wa watani wao hao, Ally Mustapha ‘Barthez’ pamoja na mabeki wake, wakikosa la kufanya.

Bao hilo liliamsha nderemo za mashabiki wa Simba waliokuwapo uwanjani hapo na kwingineko, huku likiamsha morali zaidi kwa wachezaji wa Wekundu wa Msimbazi hao waliokuwa wakipambana kuongeza la pili, huku wale wa Yanga wakichanganyikiwa zaidi.

Na iwapo kungeongezwa dakika japo tano tu, ni wazi Simba walikuwa na nafasi ya kuongeza bao la pili hata la tatu na kuondoka uwanjani na pointi zote tatu, kukata ngebe za Yanga.

Baada ya mchezo huo, kila mmoja, hasa mashabiki wa Yanga, alikuwa na lake la kusema juu ya matokeo waliyoyapata, japo mwisho wa siku wengi walionekana kumtupia lawama Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Bara, Hans van der Pluijm.

MAMBO MATANO YANAYOMSHITAKI PLUIJM

Kuchelewa kumtoa Mahadhi

Hata wakati mchezo huo ukiwa unaendelea, ilionekana wazi Juma Mahadhi kutokuwa katika kiwango chake kiasi cha kutotoa msaada wowote kwa timu, hivyo wengi walitarajia kocha huyo angemtoa na kumwingiza mchezaji mwingine, hasa winga Simon Msuva, ambaye amekuwa akianza katika mechi nyingi zilizopita.

Pia, mshambuliaji wa kati, Donald Ngoma, hakuwa katika kiwango cha juu kiasi cha kubaki kuwa msumbufu kwa mabeki wa Simba, badala ya kutafuta nafasi za kufunga na kucheka na nyavu kama ilivyokuwa kwa Tambwe ambaye kimsingi ndiye aliyekuwa moto wa kuotea mbali kwa mabeki wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Mwisho wa siku, kocha huyo akaonekana kama ndiye sababu ya kushindwa kuisambaratisha Simba Jumamosi iliyopita.

 

Kutotumia faida ya Simba pungufu

Baada ya kiungo na nahodha wa Simba, Jonas Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu, mashabiki wa Yanga wapo walioamini huenda siku hiyo ilikuwa ni nafasi yao ya kipekee kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 6-0 na watani wao hao mwaka 1977.

Lakini tofauti na ilivyotarajiwa na wengi, wachezaji wa Yanga walianza kucheza kwa mbwembwe kama vile walikuwa wakiongoza kwa idadi kubwa ya mabao na hivyo kutoa mwanya kwa wenzao wa Simba kujipanga na kurudi mchezoni.

Hapa Pluijm analaumiwa kwa kushindwa kutumia faida ya kucheza dhidi ya timu pungufu, lakini ambayo imetoka kwenye vurugu zilizofanywa na mashabiki wake.

Pluijm japo alikuwa anaongoza kwa bao 1-0 tu, bado alionekana kama alikuwa na uhakika wa kushinda japo hakuna jipya alilolifanya zaidi ya kuwaingiza Msuva na Niyonzima dakika za lala salama.

 

Kushuka viwango kwa nyota wake

Pluijm, ambaye ni raia wa Uholanzi, amejikuta akiwa lawamani kwa madai kuwa ameshindwa kuboresha viwango vya baadhi ya nyota wake, akiwamo Niyonzima, Msuva, Matheo Simon, Malimi Busungu, Geoffrey Mwashiuya, Mbuyu Twite, Said Juma Makapu, Pato Ngonyani, Paul Nonga na wengineo.

Wapo mashabiki wanaomlaumu Pluijm kwa ‘kutembelea’ uwezo binafsi wa wachezaji, lakini akishindwa kuwalinda kwa namna moja ama nyingine na mwisho wa siku, wachezaji hao kushuka viwango.

Inaelezwa kuwa tangu kocha huyo alipotua Jangwani, matatizo ya Msuva ni yale yale, huku kocha huyo akishindwa kulinda au kupandisha viwango vya wachezaji kama Mwashiuya, Matheo, Nonga, Makapu na wengineo.

 

Ubishi kwa wenzake

Habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la Yanga, zinadai kuwa kocha huyo ni mbishi asiyependa kupokea ushauri wa wenzake, kiasi cha kumponza msaidizi wake, Juma Mwambushi, anayeonekana hana msaada wowote kwenye timu.

Inadaiwa kuwa Mwambusi amekuwa akishindwa kuonyesha makali yake ya Mbeya City kwa kuwa bosi wake huyo ni mzito wa kupokea ushauri, hasa katika suala zima la kupanga kikosi na kufanya mabadiliko.

Pluijm anadaiwa kutumia uungwana wa Mwambusi kufanya kila anachotaka katika kikosi chake, tofauti na alivyokuwa akifanya wakati akiwa na Charles Boniface Mkwasa, ambaye alikuwa ‘akimdindia’ katika baadhi ya mambo.

 

Ukali kwa wachezaji

Japo wachezaji wa Yanga wamekuwa wakikanusha, lakini ukweli ni kwamba Pluijm amedaiwa kuwa mkali kwa wachezaji wake hata katika mambo yasiyokuwa na msingi.

Hali hiyo ilijionyesha Jumamosi iliyopita, wakati wa mechi dhidi ya Simba wakati nahodha wake, Vincent Bossou, alipokuwa akimsisitiza mara kwa mara kufanya mabadiliko, lakini kocha huyo hakuwa akijali.

Katika kuonyesha jinsi Pluijm alivyo mbishi na kiburi, kuna wakati Bossou alipokuwa akimsisitiza kufanya mabadiliko, alionyesha kidole chake kichwani ama kuashiria beki wake huyo hakuwa na akili au yeye alikuwa anajua kile alichokuwa akikifanya.

Mwisho wa siku, Pluijm amejikuta akiwagawa mashabiki wa Yanga, baadhi wakitaka kocha huyo kufungashiwa virago kwa madai kuwa uwezo wake umefikia kikomo, huku wengine wakipendekeza Mkwasa kurejeshwa kikosini.

Yote kwa yote, tusubiri na kuona kama si kusikia nini kitajiri Jangwani baada ya Yanga kushindwa kulipiza kisasi cha kipigo cha mabao 6-0 walichopewa na Simba mwaka 1977.

 

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -