NA JESSCA NANGAWE
KOCHA msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema kiwango cha timu hiyo kinapanda na kushuka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kutokana na wachezaji kuwa na uchovu wa Ligi Kuu Bara.
Mayanja ameliambia BINGWA kuwa hatua ya wachezaji kukosa muda wa kupumzika baada ya kushiriki ligi kuu ndiyo sababu ya kuporomoka kwa kiwango cha uchezaji wao.
Alisema pamoja na hali hiyo bado wana imani ya kufika mbali katika michuano hiyo na kuongeza kuwa wapo tayari kuikabili timu yoyote wakiwamo wapinzani wao Yanga pamoja na Azam.
“Yanga na Azam zote zinashiriki na huenda tutakutana nazo katika hatua zinazofuata, hatuna shaka yoyote kwani tumejiandaa kuzikabili,” alisema Mayanja.
Simba inaongoza kundi A ikiwa na jumla ya pointi saba huku Yanga iliyopo kundi B ikiongoza kwa kuwa na pointi 6 juu ya Azam yenye pointi 4.
Simba, Yanga na Azam huenda zikakutana kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kutokana na misimamo ya makundi yao.