NA SALMA MPELI
BAADHI ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara wameelezea jinsi walivyoguswa na kifo cha mchezaji wa timu ya vijana ya Mbao FC ya jijini Mwanza, Ismail Khalfan.
Khalfan alifariki ghafla uwanjani juzi baada ya kuanguka akiwa anaichezea Mbao FC dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa Ligi ya Vijana ya Walio Chini ya Umri wa Miaka 20 ya klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya mchezaji huyo kuifungia timu yake hiyo bao lililoisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kupitia kurasa zao mbalimba za mitandao ya kijamii,wachezaji hao wameposti ujumbe kuhusiana na kifo hicho.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayecheza Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, aliandika: “Poleni wanafamilia, timu ya Mbao FC na wanamichezo wote. Kwa kweli ni jambo la huzuni sana, lakini kazi ya Mungu haina makosa, tumuombe apumzike salama”.
Naye mshambuliaji wa Yanga, Deus Kaseke, aliandika: “Pumzika kwa amani Ismail Khalfan, poleni Mbao FC, poleni familia na sisi sote wanafamilia ya mpira”.
Simon Msuva ambaye ni winga machachari wa Yanga, aliandika: “Pumzika kwa amani kaka, napenda kutoa pole kwa timu ya Mbao FC, ndugu, jamaa na marafiki, mbele yetu nyuma yake”.
James Msuva, anayechezea JKT Ruvu ya Pwani, aliandika: “Goli zuri, ulishangilia vizuri, kumbe ndio ulikuwa unatuaga dah, mbele yetu nyuma yako, kapumzike kwa amani Khalfan, ni ngumu kuamini ujue, ila ndiyo kazi ya Mola”.
Jerryson Tegete, ambaye ni mshambuliaji wa Toto, aliandika” “Ni huzuni sana, pumzika kwa amani dogo Ismail na kila nafsi itaonja umauti, tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu mlichonacho Mbao FC”.
Kipa wa Azam, Aishi Manula, aliandika: “Ni pigo kubwa kwa wanamichezo na Watanzania kwa ujumla, kwani alikuwa kijana ambaye mwanga wa mafanikio ulikuwa juu yake, ila kazi ya Mola huwa haina makosa”.
Nahodha wa Kagera Sugar, George Kavilla, aliandika: “Pumzika kwa amani Ismail Mrisho, hakuna mwanadamu anayeweza kuushinda mtihani huu, pole kwa ndugu, marafiki, wapenzi na timu ya Mbao FC kwa msiba huu, jina la Bwana libarikiwe”.