NA MWANDISHI WETU
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika Klabu ya Genk nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta, leo atakuwa uwanjani timu yake itakapocheza na Athletic Club ya nchini Hispania katika mfululizo wa michuano ya Europa League.
Kikosi hicho cha akina Samatta kitakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Luminus Arena, kuwakabili vigogo hao wa Hispania ambapo kama wakishinda wanaweza kuongoza ligi hiyo.
Genk na Athletic wapo Kundi F sambamba na SK Rapid Wien ya Austria na Sassuolo ya Italia, ambapo kila timu ina pointi tatu kila moja.
Katika msimamo huo wa Kundi F, Athletic wanaoongoza wakiwa na uwiano mzuri wa mabao huku Genk ikifuatia, SK Rapid wakishika nafasi ya tatu na Sassuolo wakiwa nafasi ya nne.
Athletic Club inashika nafasi ya saba Ligi Kuu ya Hispania kutokana na pointi 15 baada ya kucheza mechi nane huku Genk wakiwa nafasi ya tisa kwa pointi 14 katika mechi 10 za Ligi Kuu nchini Ubelgiji.