ROMA, Italia
TIMU ya Udinese imeamua kumtimua kocha wake, Giuseppe Iachini, ikiwa ni siku moja baada ya kuambulia kipigo cha mabao 3-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Lazio.
Hatua hiyo imekuja baada ya timu hiyo kucheza mechi nne bila kupata ushindi na kufanya ishuhudiwe klabu hiyo ya Stadio Friuli ikiwa miongoni mwa timu zinazoshika nafasi za mwisho katika msimamo wa Ligi ya Serie A.
Udinese ilimkabidhi mikoba hiyo Iachini kwa ajili ya msimu huu, ikiwa ni baada ya kunusurika kushuka daraja msimu uliopita.
Hata hivyo, pamoja na kumtimua, timu hiyo ilimshukuru kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 kwa kazi aliyoifanya katika mechi nane.
“Hata hivyo, tunamshukuru Iachini kwa kazi aliyoifanya Udinese Calcio, tunamtakia kila la kheri katika kazi yake,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
Hadi anakabidhiwa timu hiyo, kocha huyo aliwahi kuifundisha Palermo mara mbili.