NA WINFRIDA MTOI
KOCHA wa zamani wa timu ya Ndanda FC, Abdul Mingange, amepanga kuukomesha uongozi wa klabu hiyo ikiwa utamwita tena kukisaidia kikosi kitakapokuwa katika janga la kushuka daraja.
Mingange ambaye aliinusuru Ndanda kushuka daraja katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, kwa sasa ametupiwa virago na nafasi yake kuchukuliwa na kocha mwingine.
Akizungumza na BINGWA, Mingange alisema kama atafuatwa kwa mara nyingine timu ikiwa katika hali mbaya atatoa masharti magumu ya kurudi kwa sababu hajaridhishwa na kitendo cha kumwondoa kwenye benchi la ufundi.
Alisema kuwa anaipenda Ndanda ndio maana inapokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja akiitwa haoni tabu kuipigania na amefanya hivyo kwa misimu miwili.
“Ndanda ni timu yangu na mara kwa mara wananiita timu inapokuwa katika hali ngumu na ninakubali bila kujali mambo ya fedha, lakini mara nyingine ni lazima nitoe masharti kutokana na kitendo walichonifanyia,” alisema Mingange.
Hata hivyo, Mingange alisema kwa sasa timu yoyote ambayo itamhitaji atakuwa tayari kufundisha hata kama inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), kwani jambo la msingi ni kuzingatia mahitaji yake.
“Ukocha ni kazi yangu, hivyo timu yoyote ya Ligi Kuu au daraja la kwanza ikinihitaji nitafundisha, labda isiwe na uwezo wa kutoa huduma zote nitakazotaka kama ilivyokuwa Singida United,” alisema.