NA ZAINAB IDDY
BAADA ya Yanga kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao mbili, nyota wa zamani wa klabu hiyo, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, amesema safu ya ushambuliaji ndio wanapaswa kutupiwa lawama.
Yanga imecheza jumla ya mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, wakitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli FC kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, kabla ya kuichapa Mji Njombe bao 1-0 wiki iliyopita.
Mabingwa hao watetezi waliambulia sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Majimaji FC mjini Songea na kumfanya Mmachinga kumtaka kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, afanye maamuzi magumu.
Akizungumza na BINGWA juzi, kwenye Uwanja wa Taifa, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Simba dhidi ya Mwadui FC, ambao Wekundu wa Msimbazi walishinda 3-0, Mmachinga alisema tatizo kubwa lililopo Yanga ni safu ya ushambuliaji, ambayo wachezaji wake wanaonekana kuchoka kuitumikia timu hiyo.
“Ukianza kumwangalia Donald Ngoma unaweza kusema analazimishwa kucheza, kwani si yule wa misimu miwili iliyopita, hali ambayo ipo pia kwa Juma Mahadhi,” alisema Mmachinga.
“Amis Tambwe kila siku ni majeruhi, hivyo Yanga imebaki na washambuliaji wawili pekee wanaojituma, ambao ni Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa, nao hawawezi kuisaidia timu kwa asilimia 100, kwani wao pia wanahitaji kusaidiwa.
Mmachinga anasema jambo la maana kufanya ni kuchukua uamuzi mgumu wa kuwaacha dirisha dogo la usajili na kuchukua wengine ambao watakuwa tayari kuisaidia Yanga.