Friday, September 25, 2020

Mo Dewji afunga mjadala

Must Read

Azam FC yakiri Mbeya City kiboko

NA WINFRIDA MTOI LICHA ya kuchukua alama tatu kwa Mbeya City, uongozi wa Azam...

Niyonzima ala kiapo mechi za ugenini

NA ZAINAB IDDY NAHODHA msaidizi wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kuwa mipango ya timu...

Yanga achana nao

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga umekuja na mkakati maalum wa kuhakikisha wanakusanya pointi...

WINFRIDA MTOI

HATIMAYE Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, amefunga rasmi mjadala juu ya mambo mbalimbali ndani ya klabu hiyo, yaliyokuwa yakiumiza vichwa vya mashabiki, wanachama na wapenzi wao kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo hayo ni suala la kufukuzwa kwa kocha Patrick Aussems, mrithi wake, sababu za kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, suala la utovu wa nidhamu, mwelekeo wao na msimamo wa klabu hiyo juu ya yote hayo na mengineyo.

Nidhamu

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanachama uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, Mo alisema kuwa amekuwa haridhishwi na nidhamu ya baadhi ya wachezaji wao nje ya uwanja.

“Siridhishwi hata tone na nidhamu ya baadhi ya wachezaji wetu nje ya uwanja. Nimekuwa mnyonge kuona uwekezaji tuliouweka kwao, baadhi yao, huutumia kama fimbo ya kutuchapia.

“Niwaambie wachezaji wote, Simba ni klabu kubwa kweli kweli, tena kubwa hasa, na hakuna shaka ni namba moja Afrika Mashariki, bodi ninayoiongoza mimi haitavumilia mchezaji yoyote asiyejua thamani ya Simba. Kuonyana onyana sasa imetosha.

“Sisi tunawalipa vizuri mno, na wao wana wajibu wa kutulipa matokeo na furaha. Na ili furaha iwepo, lazima nidhamu isimamiwe kikamilifu na katika hili, hatutanii. Hatutajali ukubwa wa jina la mchezaji yoyote,” alisema Mo Dewji.

Aliongeza: “Simba lazima tuamue kuteseka na moja katika mambo haya mawili, mosi tuzoee uchungu na maumivu ya nidhamu au maumivu ya matokeo mabaya. Kama mpenzi wa Simba, siwezi.”

Kauli hiyo ya Mo Dewji ni salamu tosha kwa wachezaji waliokuwa wakishutumiwa kwa madai ya utovu wa nidhamu, wakiwamo viungo, Jona Mkude na Clatous Chama.

Msimamo wa Simba

“Msimu huu wa ligi, tutahakikisha tunachukua tena ubingwa ili tuje kuweka rekodi nyingine kwenye Afrika. Nawahakikishia wanachama wenzangu, kujikwaa si kuanguka, hatutarudia makosa.

“Tuna mpango wa kufungua Simba ‘academy’ ili hapo badaye tuje kuvuna vijana waliolelewa kwenye asili ya Simba. Tuwafundishe vijana hao thamani ya Simba na falsafa ya uchezaji wa Simba, sambamba na upendo ili wawe na uchungu zaidi na klabu yetu.”

Kufukuzwa kwa Aussems

Mo Dewji alisema kuwa uamuzi huo ulitokana na klabu yao kutoridhishwa na mweneno wa kikosi chao ndani na nje ya uwanja.

“Niliumia sana kupoteza mechi iliyoandaliwa na wadhamini wetu Sportpesa, ambayo tulicheza na klabu kubwa ya Sevilla kutoka Hispania. Ile mechi tulikuwa tushaongoza kwa idadi nzuri ya magoli, lakini kilichotokea hadi sasa sielewi.

“Tulipata shida kidogo msimu huu. Nikisema ni bahati mbaya ni utetezi dhaifu, itoshe kusema yaliyotokea msimu huu Ligi ya Mabingwa Afrika ni fundisho kwetu, na nadhani hatupaswi kurudia makosa tuliyoyafanya. Ilikuwa ni aibu kwetu, na tulijiangusha,” alisema Mo Dewji.

Aliongeza: “Binafsi bado sijakaa sawa hadi leo baada ya matokeo ya mechi yetu dhidi ya timu ya UD Songo. Nilikuwa sipo nchini. Baada ya mechi ile kuisha, nililia mno.”

Alisema hata kitendo cha Aussems kushindwa kusimamia nidhamu ya wachezaji wake, nacho kilichangia kufukuizwa kwake.

“Nidhamu kwetu ni muhimu kama tunataka tufikie malengo tuliyokusudia. Na haya ndio yaliyotufanya bodi tuchukue maamuzi magumu kwa kocha wetu. Timu imeshindwa kufikia malengo, kisha nidhamu hakuna, halafu tuvumilie?”

Hataki kufungwa wala sare

Mo Dewji alisema japo anafahamu katika soka kuna matokeo matatu, yaani ushindi, sare na kufungwa, lakini kuanzia sasa hayupo tayari kusikia timu yao hiyo inapoteza pointi hata moja.

“Nataka klabu hii, iwekeze katika tokeo moja tu, la ushindi. Bado sijaridhishwa sana na mwenendo wetu katika ligi ya nyumbani, hata kama tunaongoza ligi. Simba inapaswa icheze kama bingwa mtetezi na kwa soka letu lenye kuburudisha na kutoa matokeo sahihi.

Mrithi wa Aussems

“Tunaleta kocha mkubwa, ana rekodi za maana, ni nchi gani anatokea subirini mtatangaziwa  muda si mrefu, lakini mfahamu anaendana na ukubwa wa klabu ya Simba,” alisema Mo.

Vipi kuhusu Mo Simba Arena?

Kuhusu uwanja wa mazoezi wa Bunju ambao kwa sasa unaitwa Mo Simba Arena, alisema ujenzi uliokamilika ni awamu ya kwanza na mambo mazuri yanakuja.

Alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.5 za Kitanzania, kuanzia kama mwanachama atachangia milioni 500.

“Kiasi kilichobaki tutafanya harambee ili kupata fedha inayotakiwa, bila shaka tutafanikiwa ili msimu wa 2021/22 tukae kwenye hosteli zetu. Kazi yangu ni kuhakikisha wachezaji wanapata mazingira bora na mishahara mizuri, waweze kufanya kazi vizuri,” alisema.

Mazingiza afunguka

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Senzo Mazingiza, alisema hadi sasa wamefikia pazuri kutokana na kulipa mishahara na kutoa posho kwa wakati.

“Wachezaji wetu wanalipwa vizuri ukilinganisha na klabu kama Azam na Yanga, kiwango cha fedha kinachotumika katika usajili na masuala mengine ya uendeshaji wa klabu ni kikubwa.

“Haya ni maendeleo muhimu barani Afrika, ni klabu chache zinaweza kumudu hatua hii kwani Simba ni timu kubwa katika soka la Afrika hivyo ni jukumu letu sote, hasa kwa wachezaji kufanya vizuri ndani ya uwanja na kuifanya iendelee kutambulika kama klabu kubwa.

“Usajili wa wachezaji utafanyika kwa namna tofauti, tutatoa mikataba mirefu kwa wachezaji kwa kuzingatia utaratibu wa kitaalamu, kama unataka kucheza hatua ya nusu fainali kimataifa unahitaji kikosi kitakachoweza kukaa pamoja kwa miaka mitatu hadi minne,” alisema Mazingiza.

Atuma salamu Yanga

Mazingiza alisema: “Nafahamu tuna mchezo muhimu na watani wa jadi Januari, napenda kuwahakikishia kuwa maandalizi na mambo yote yapo vizuri, wachezaji watakuwa kambini na tangazo la nani atakuwa kocha mkuu mpya na benchi la ufundi litatoka rasmi Jumatano.”

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Azam FC yakiri Mbeya City kiboko

NA WINFRIDA MTOI LICHA ya kuchukua alama tatu kwa Mbeya City, uongozi wa Azam...

Niyonzima ala kiapo mechi za ugenini

NA ZAINAB IDDY NAHODHA msaidizi wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kuwa mipango ya timu yao ni kuwa na mwendelezo...

Yanga achana nao

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga umekuja na mkakati maalum wa kuhakikisha wanakusanya pointi tatu kila mchezo, wakianzia mechi...

CHAMA GUMZO KILA KONA

NA WINFRIDA MTOI KIWANGO kilichoonyeshwa na kiungo wa Simba, Clatous Chama katika mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania...

United ‘kimeo’ yamtoa povu Evra

MANCHESTER, EnglandBEKI wa zamani wa Manchester United, Patrice Evra, amekerwa na namna mambo yanayoendelea katika klabu hiyo, hasa ishu za usajili.
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -