NA SALMA MPELI
WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, jana alikwea pipa na timu yake mpya ya Difaa El Jadida ya Morocco kwenda nchini Hispania kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu nchini humo.
Msuva ambaye ameuzwa na Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga kwenye klabu hiyo ya Morocco, hadi sasa ameshaichezea mechi mbili za kirafiki na kufanikiwa kuifungia timu yake hiyo mpya mabao matatu.
Akizungumza na BINGWA jana kwa simu kutokea nchini humo, Msuva alisema wanakwenda Hispania kwa kambi ya maandalizi ya siku saba ambapo watacheza mechi tatu za kujipima nguvu.
“Tunakwenda huko na tutakaa siku saba, kwa mujibu wa kocha tutacheza mechi tatu za kirafiki tukiwa huko, lakini bado sijajua ni timu gani tutacheza nazo,” alisema Msuva.
Msuva ambaye alicheza Yanga kwa mafanikio makubwa tangu alipotua kwenye kikosi hicho msimu wa 2012/13, ameondoka akiwa na tuzo mbili za ufungaji bora akitwaa kwa misimu miwili mfululizo, 2015/16 na 2016/17 huku akiisaidia timu yake hiyo kutwaa Kombe la Ligi Kuu mara tatu mfululizo.
Mchezaji huyo ataonekana kwa mara ya kwanza kwenye ligi ya nchini Morocco msimu ujao, akiwa na kikosi cha timu hiyo ambayo msimu uliopita kimemaliza kikiwa kwenye nafasi ya pili katika msimamo wenye jumla ya timu 16.