NA ZAINAB IDDY
YANGA imeonekana kukosa kasi yake ya msimu uliopita, lakini winga wa timu hiyo, Simon Msuva, amesema bado hawajakata tamaa kwenye mapambano ya kuwania taji la ubingwa msimu huu.
Yanga inakamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kucheza mechi nane, ikishinda nne, sare tatu, huku ikipoteza mchezo mmoja na kujikusanyika pointi 15.
Simba ambao ni wapinzani wakubwa wa Yanga, wao wanakamata usukani wa ligi hiyo baada ya kushuka dimbani mara tisa, wakishinda michezo saba na kutoka sare mbili.
Akizungumza na BINGWA jana, Msuva alisema bado wana michezo mingi mkononi ambayo kama watapata matokeo mazuri na wenzao walioko juu kuharibu wanaweza kukalia kiti cha uongozi na kutwaa ubingwa.
“Najua mashabiki wanaumizwa na matokeo tunayopata, hata sisi wachezaji, benchi la ufundi na viongozi hatufurahii lakini wakati mwingine mpira uko hivyo.
Mpira una matokeo matatu, kushinda kufunga na sare lakini muhimu kwetu ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye michezo yetu inayofuata.
“Nawaomba mashabiki waendelee kutuunga mkono wasikate tamaa kwani ni mapema sana, ukweli ni kwamba ligi ni ngumu na kila mtu anaona, tunachowaahidi tutaendelea kujituma ili tuweze kufanya kile wanachokiitaji,” alisema Msuva.